Suala la Uhuru ni muhimu sana kuanzia ngazi ya mtu binafsi, makabila, majimbo, mataifa na hatimaye dunia kwa ujumla. Ni kutokana na umuhimu wa uhuru ndio maana baadhi ya nchi zimefikia hatua ya kumwaga damu kwa ajili ya kujitafutia uhuru. Zipo nchi ambazo mpaka sasa watu wake wanapambana kufa kupona ili wajikomboe kutoka kwenye unyanyasaji na mateso yatokanayo na Ukoloni ili waweze kuyafaidi matunda ya raslimali walizopewa na Mungu.
Migogoro itokanayo na kudai uhuru siku zote inapingwa vikali na wale wanaosemwa kuwa ni waonevu au wakoloni. Hii inatokana na ukweli kwamba ipo imani kwamba ukubwa wa ardhi inayomilikiwa na nchi fulani ni kipimo cha ubora wa uchumi kwa kuwa ardhi inajumuisha ndani yake raslmali nyingi ambazo zinathamani na manufaa makubwa kwa nchi. Lakini pia kwa upande wa pili wa shilingi kuna sababu za msingi ambazo hutolewa na hao wanaohitaji uhuru au kujitenga ambazo huwa na lengo la kuonyesha umuhimu wa kufanya hivyo.
Tatizo kubwa katika migogoro kama hii ni lile litokanalo na maana ya neno ‘Ukweli’, haswa ikizingatiwa kwamba mwanadamu ni kiumbe mwenye hila nyingi na mwenye uwezo wa kufanya mambo kinyume lakini akajenga hoja ili kuwaonyesha wengine kwamba anayoyasema ni ya kweli na kwanamna moja ama nyingine aweze kupata msaada kutoka kwa wenzake. Ndio maana harakati zote duniani huanza na mtu ama kikundi cha watu na kuendelea kukua kadri siku zinavyokwenda.
Suala la kudai uhuru linaendana kwa kiasi kikiubwa na uzalendo, lakini sio kila anayepigania uhuru ni mzalendo na hii ndio maana kuna waasi kama akina Joseph Kony wa Uganda na wengine wengi. Hawa hatuwezi kuwaita wazalendo kwa kuwa wanachokifanya ni uvunjifu wa haki za binadamu, suala la kuwalazimisha watoto kujiunga na jeshi kwa kisingizio cha kudai uhuru au kuwatesa wanawake na watoto na kuwaua wananchi kwa kisingizio cha kumshurutisha mtu kuachia madaraka sio katika vitendo vya kizalendo.
Tukirudi kwenye nchi yetu, tayari kunajinamizi linafukuta chini kwa chini kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Baadhi ya wanahistoria na wachambuzi wa mambo wanadai kwamba Muungano wetu ulikuwa wa muda mfupi na kwa hiyo ipo sababu ya kupitia upya kwa umakini vipengele vya muungano ili kuona kama ipo haja ya kuendelea kua nao kama ulivyo au kuangalia uwezekano wa kuuboresha zaidi ili uwe na usawa baina ya pande mbili. Hii inatokana na madai kwamba upande wa pili wa Muungano haswa Zanzibar haufaidi vyema matunda ya Muungano jambo linalowapelekea baadhi ya watu kudai kwamba muungano hauna tija kwao.
Nivigumu kugundua ukweli uliopo ndani ya madai haya kwa kuwa mwanadamu kwa asli ni mtata na anapenda kuvutia kwake, wakati Wazanzibar wanalalamika kwamba hawatendewi haki ndani ya Muungano, Serikali ya Tanzania inakanusha vikali kwa kutoa ushahidi wa mambo mbalimbali ambayo yanafanywa na Serikali huko Zanzibar yenye malengo ya kuboresha maisha ya watu jambo linaloonyesha kwamba upo usawa au kwa maneno mengine zipo jitihada za kuleta maisha bora sio kwa Watanganyika tu bali na kwa Wazanzibar pia.
Lakini ikiwa mataifa dhaifu Duniani yanapigana kwa udi na uvumba kuhakikisha kwamba yanapata maeneo zaidi ya kujiunga ili yawe na nguvu, haifahamiki ni kwanini baadhi ya Wazanzibar wanataka kujitenga kutoka kwenye Muungano wa sasa. Lakini pia haijulikani ni kwa jinsi gani ambavyo Wazanzibar wamejipanga kujiletea maendeleo binafsi kama nchi watakapotengana na Tanganyika. Hii inatokana na ukweli kwamba tayari tunaiona Zanzibar yenye mpasuko mkubwa wa kisiasa, kijamii na kiuchumi jambo linalosababisha tuamini kabisa kwamba Zanzibar sio moja na kama sio moja haiwezi kuendelea hata kama itajitenga kwa kuwa pasipo umoja hapana nguvu.
Ni hivi majuzi, tumeshuhudia kundi la watu 12 kutoka Kisiwa cha Pemba wakiwasilisha barua yao ya kuomba uhuru wa kisiwa hicho kwenye ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini, Oscar Fernandez. Wapemba hao wanadai kwamba wameandika barua hiyo kwa kuzingatia kwamba hakuna historia inayoonyesha kwamba Kisiwa cha Pemba kiliwahi kuungana na Kisiwa cha Unguja na hivyo wameonelea ni bora waombe uhuru wa kisiwa hicho kutoka Umoja wa Mataifa. Lengo lao kuu wanataka Serikali ya Tanzania ishurutishwe na Umoja wa Matifa kuipatia Pemba uhuru wa kuunda Serikali yake.
Watu hao ambao walidai kwamba wametumwa kwa niaba na kundi la Wapemba wapato 10,000. Wanasema walichokidai ni cha msingi kabisa kwa kuwa ni jambo ambalo lipo na mfano wanao kutoka kwenye Visiwa vya Comoro ambako kila Kisiwa kina Serikali yake ambavyo vinaunganishwa na Serikali Shirikishi. Lakini suala linalozua utata zaidi ni kwamba wanadai wamepeleka kilio chao hicho UN ili Katibu Mkuu wa Umoja huo aingilie kati kwa lengo la kuwapa haki zao za kimsingi na kuwasaidia kuepukana na matatizo ya kiubaguzi.
Lakini suala la Umoja wa Mataifa kuingilia kati mgogoro wa nchi linakuja mara baada ya nchi husika kushindwa kufikia maamuzi ya matatizo yanayoikabili. Je wenzetu wanataka kusema kwamba Serikali ya Tanzania ilishaombwa kuwapa uhuru Wapemba ikakataa? Na kama hawajawahi kuyapeleka maombi hayo Serikalini yakakataliwa ni kwanini haswa wanautaka Umoja wa Mataifa uingilie kati? Maswali haya pengine ndiyo yameipelekea Serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshugulikia Muungano Mh. Muhammed Seif Khatib kukiita kitendo hicho kwamba ni cha uhaini kwa kuwa kinalenga kuipindua nchi.
Kimsingi Wenzetu Wazanzibar wanamatatizo mengi na jambo hili halifichiki hata kidogo, lakini inafahamika fika kwamba mchakato ungali ukiendelea wakuitafutia Zanzibar ufumbuzi wa matatizo japo hali ingali tete. Hivyo basi suala la kuongeza matatizo juu ya matatizo sio la busara kabisa. Hii inatokana na ukweli kwamba ilitegemewa kwamba Wazanzibar sasa wangeungana na kumpiga adui “Mpasuko” ili kurejesha hali ya amani ambayo tayari emefika njia panda. Lakini badala yake wenzetu ndio kwanza wanapeleka barua UN kuomba uhuru wa Pemba hata kabla ya kulimaliza hili la mpasuko. Hali hii inaleta mkanganyiko wa mambo na pengine isiwasaidie sana Wazanzibar.
Lakini pia kwa anayewafahamu vizuri Wazanzibar atapata wakati mgumu kidogo kuelewa kwamba ni nini haswa ambacho wanakitaka. Je wanataka Serikali ya mseto?, Kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar?, au Kupata uhuru wa Pemba? Haya ni mambo ambayo yanakinzana sana na yanaonyesha kabisa kwamba watu hao bado hawajui wanachokitaka.
Hapa Tanzania ukiyataja makabila matano ambayo yanaongoza kwa utajiri, basi Wapemba wamo. Tena wametapakaa kila sehemu nchini kote na wanafanya kazi bila kuulizwa viza kwa kuwa ni Watanzania wenzetu. Lakini hebu tujiulize ikiwa mambo yako hivyo kwanini wapemba wanahisi kwamba Wametengwa? Pia wachunguzi wa hali ya mambo wanasema kwamba Wapemba wengi kwa sasa wamesoma sana wakilinganishwa na Waunguja, sasa kwanini wahisi kwamba wametengwa? Pia ni ukweli usiopingika kwamba Wapemba wengi wapo Ulaya na wanamaisha mazuri sana huko, kwa wanaowafahamu wanasema kwamba wapo ambao tayari wameanzisha vijiji vyao huko Uingereza, Kanada, Dubai na maeneo mbalimbali Duniani. Je kwa yote haya kwanini watu hawa wahisi kwamba wametengwa?
Ukweli ni kwamba Zanzibar imara itajengwa na Wazanzibar wenyewe, hivyohivyo Pemba imara itajengwa na Wapemba wenyewe na Unguja imara itajengwa na Waunguja wenyewe. Niliwahi kunukuu msemo mmoja wa Kihaya usemao kwamba mtoto yatima akifikia hatua ya kubaleghe moyo wake tayari unakuwa umeshaota mvi. Msemo huu unamantiki kubwa sana haswa ikizingatiwa kwamba kadri mwanadamu anavyopitia hali ngumu kimaisha, yeye huzidi kuwa madhubuti na hujenga uwezo mkubwa wa kuyahimili matatizo yake. Lakini anapokua tegemezi hubweteka na kusubiria afanyiwe kila kitu.
Hali ya Zanzibar nionavyo mimi haina tofauti sana na ya Mkoa wa Dar es Salaam unapoulinganisha na mkoa wa Pwani. Mikoa hii miwili ipo karibu sana lakini inatofautiana kimaendeleo kwa mbali sana. Hii haimaanishi kwamba Pwani imetengwa na Dar es salaam inapendelewa, lakini zipo sababu za kihistoria, kiuchumi, kijamii na kisiasa ambazo zinaupelekea mkoa wa Pwani kuwa nyuma kimaendeleo. Ni ukweli usiopingika kwamba miji yote mikuu ya Afrika imeendelea sana ikilinganishwa na miji mingine na hii inatokana na ukweli kwamba kwenye maendeleo ndiko wanakopenda kuwekeza watu kwa kuwa hata miundombinu huwa ipo imara na matokeo yake miji iliyobaki nyuma inazidi kuwa nyuma na iliyoendelea inazidi kuendelea.
Tanzania nzima imekaa kimatabaka kutokana na mifumo iliyowekwa tangu zama za Wakoloni, miji iliyoendelezwa na wakoloni imezidi kuwa mizuri kadri siku zinavyosogea na ile iliyokuwa nyuma bado ingali ikijikongoja. Mpaka leo kunabaadhi ya Makao Makuu ya Wilaya hapa nchini hayana umeme wa kuaminika. Ni miaka ya hivi karibuni ndio tumeshuhudia kujengwa kwa barabara inayounganisha Kusini mwa Tanzania na Dar es salaam, kabla hali ilikuwa mbaya sana. Lakini hatukuwahi kuwasikia watu wa Lindi na Mtwara wakiomba kujitawala kwa kisingizio cha kutengwa. Hata hivyo wamevumilia na hatimaye wamefikia pazuri sasa.
Kwa bahati mbaya viongozi wetu wa kisiasa wanafikiri kwamba madaraka ni muhimu sana kushinda mustakbali wa wananchi na nchi kwa ujumla. Inafikia pahala watu wanataka kupewa uhuru wa kujitawala ili ndugu zao wawe maraisi na kwa kuwa wanajua fika kabisa kwamba Mawaziri watatoka miongoni mwao, pia wanajua kabisa kwamba ikishakua nchi itapata ruzuku na misaada kutoka nje kwa kigezo cha kusaidia shughuli za kimaendeleo na humo mafisadi nao watapata kujichotea vijisenti vyao. Lakini kwa faida gani haswa?
0 comments on Wazanzibar wanataka nini?
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster








