'United States of Africa' Kitendawili Kigumu

June 2, 2008 / by saiboko

Umoja ni nguvu ni msemo uliozoeleka kwenye vinjwa vyetu. Ni msemo wenye mantiki kubwa ambao pia unafananishwa na misemo mingine kama ule usemao “kidole kimoja hakivunji chawa”. Misemo hii inatupa somo la ushirikiano kwa kuwa siku zote mwanadamu kwa asili yake ni kiumbe anayehitaji msaada haswa anapokumbwa na matatizo.

 

Mataifa mengi Duniani kwa kutambua umuhimu wa msemo huu yameungana ili kujiwekea wigo mpana zaidi wa raslimali watu na zile za asili. Ni ukweli usiopingika kwamba mataifa mengi ambayo yameungana yameonyesha kuwa na mafanikio makubwa kiuchumi na kijamii.

 

Historia inatuonyesha kwamba zipo nchi ambazo ziliungana zikawa na nguvu kubwa na zikawa tishio kwa mataifa makubwa kiuchumi Duniani. Mfano mzuri ni muungano uliokuwa unaziunganisha nchi za  Kisovieti chini ya Union of Soviet Socialist Republics (USSR) mungano huu ambao historia inaonyesha kwamba uliundwa rasmi Desemba 1922 ukiwa na makao yake makuu nchini Mjini Moscow Urusi, uliweza kukukua na kuchukua sehemu kubwa ya Bara la Ulaya kiasi cha kuyaogofya mataifa yote ya Dunia haswa yale amabayo yalipakana na nchi zilizokuwa ndani ya Umoja huo.

 

Historia inaonyesha kwamba kushindwa kwa chama cha Nazi cha Ujerumani kwenye vita ya pili ya Dunia ya mwaka 1939-1945 kuliifanya Jumuia hiyo ya Kisovieti kukita mizizi yake kwenye maeneo mengi zaidi japo baathi ya maeneo hayakutambuliwa na nchi za kimagharibi. Mpaka 1945 USSR ilikuwa ni nchi kubwa kuliko zote Duniani. Historia inaotuleza kwamba jumla ya ukubwa wa eneo lilokuwa linamilikiwa na USSR ilikuwa ni Kilometa za Mraba 22,402,000 ukubwa ambao unafananishwa na moja ya sita ya ukubwa wa ardhi ya Dunia nzima.

 

USSR iliifanya Urusi kukuwa kiuchumi haswa ikizingatiwa kwamba mji wake mkuu wa Moscow ndio ulikuwa makoa makuu. Mpaka inafikia mwaka 1989 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kuvunjika kwa umoja huo Moscow ilikuwa na wakazi wapatao milioni 9, pia kulikuwa na viwanda vikubwa na maendeleo ya kisayansi. Miji mingine ya umoja huo nayo ilikuwa na wastani wa wakazi milioni  moja mpaka laki tano wakiwa wanafanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Lakini kuvunjika kwa USSR mwaka 1990 kumezirudisha sana nyuma kimaendeleo nchi za umoja huo jambo linaoloonyesha kwamba kukosekana kwa umoja wa awali ndio tatizo. Huku Urusi ikiendelea kufurahia matunda yaliyovuna ndani ya USSR.

 

Tukiachana na umoja huo wa USSR ambao kwa sasa ni historia, bado tunashuhudia nguvu ya Marekani chini ya (United States of America) na pia tunaishuhudia nguvu ya Uingereza chini ya (United Kingdoms). Hii ni mifano hai ambayo ipo, mifano hii inatuonyesha kwamba kuungana ni kitu chema.

 

Tukiondoka huko kwenye mataifa ya watu, ni bora tukarejea nyumbani sasa ili tujadili ni kwa namna gani haya yanaweza kutendeka. Hivi karibuni kulikuwa na mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika huko Arusha kwenye Hoteli ya Ngurdoto, mkutano huo wa siku mbili wa Kamati Maalumu ya Wakuu wa Nchi 12 za Umoja wa Afrika (Committee of Twelve) ulilenga kujadili juu ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Afrika.

 

Kwenye mkutano huo Mwenyekiti wa AU, Rais Jakaya Kikwete alisema kwamba kimsigi nchi zote za Afrika zinakubaliana juu ya kuundwa kwa Serikali hiyo, pia wanakubaliana kwa kauli moja kabisa kwamba kuna umuhimu wakuwapo kwa Serikali itakayowaunganisha wana wa Afrika wote. Lakini bado tofauti kubwa inakuja kwenye suala zima la namna ya kufikia kwenye azima hiyo. Akifafanua juu ya jambo hili Rais Kikwete alisema kwamba wapo wanaotaka mambo yaende harakaharaka na wengine wanataka yaende hatua kwa hatua.

 

Bila shaka viongozi wetu wa Afrika ikiwa wana nia njema, wanataka kuiona Afrika moja ambayo itakuwa na nguvu kubwa kiuchumi na kisiasa, Afrika ambayo itayashughulikia matatizo yake kwa pamoja chini ya mwavuli mmoja wa ‘United States of Africa’.

 

Ndoto hii ya viongozi wetu wa Bara la Afrika inavutia sana, lakini suala la Afrika yetu kama tunavyoifahamu ni Bara la matatizo, ni bara la njaa, magonjwa, vita na siasa chafu. Matatizo yetu ni mengi tukisema tuyaunganishe huenda yakafika Antarctica huko kwenye bara lisiloishi watu. Suala hili linawataka viongozi wetu kufikiria kwa marefu na mapana kabla ya kusema ndio au hapana kwa Serikali ya Umoja wa Afrika.

 

Umoja wa Afrika ni kielelezo tosha cha kuonyesha endapo tunahitaji kuwa na Taifa moja la Afrika au la. Je tumeshakaa na kujaribu kutathimini namna ambavyo AU zamani ikiitwa OAU ilivyoweza kuyasimamia na kuyatatua matatizo ya Bara la Afriaka tangu ilipoundwa huko Addis Ababa Mei 25, 1963? Je kama matatizo ya Afrika yangali yakiongezeka kila uchao ndani ya AU ni kwanini?

 

Ukweli ni kwamba kama alivyowahi kuzungumza Mwenyekiti wa AU Rais Kikwete, matatizo ya Afrika hayatakwisha ikiwa viongozi wa Bara hili watashindwa kuacha kando tamaa za kujilimbikizia mali wakiwa madarakani na kusahau kwamba uongozi ni utumishi wa Umma. Tatizo hili bado lingani kubwa miongoni mwa viongozi wetu jambo linalopelekea watu kukosa imani na wazo hili la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika.

 

Inafahamika fika kwamba miongoni mwa viongozi wa Afrika wanaotaka Serikali ya Umoja wa Afrika iundwe mara moja ni pamoja na Rais wa Libya Muamar Gadafi ambaye misimamo yake kiutawala inaeleweka vizuri. Gadafi alipoitembelea Uganda kwenye mienzi ya hivi karibuni alikozindua msikiti mkubwa uliojengwa kwa msaada wake, alisema kwamba viongozi wa Afrika walioingia madarakani kwa mtutu wa bunduki kama  yeye hawatakiwi kiuondoka madarakani ila kwa mtutu wa bunduki. Hii ndio kusema kwamba Gadafi anawaasa akina Mugabe na Museveni wakae madarakani milele bila kujali kwamba wananchi wanawataka au hawawataki kwa kuwa waliingia ikulu kwa mtutu. Wapo waliomlaani Gadafi kwa kauli hizo na kusema kwamba wanamshangaa Museveni kumkirimu mtu mwenye kauli kama hizo bila kujua kwamba Gadafi alikuwa anayarudia maneno ya Museveni ambaye alisema kwamba hataweza kuyaachia madaraka aliyoyapata kwa taabu.

 

Kina Gadafi na Museveni wanawawakilisha viongozi wengi wa Afrika ambao hawawezi kungatuka madarakani bila mtutu wa bunduki kwa kuwa wao kuwa madarakani ni muhimu sana ili waweze kuitafuna nchi vizuri. Ni Museveni huyuhuyu ambaye alikuwa anataka Shirikisho la Afrika Mashariki liundwe harakaharaka, tukabaki tunaulizana kulikoni? Kumbe alikuwa anania ya kutaka kuwa Rais wa kwanza wa Shirikisho hilo endapolingeundwa. Nani anajua lengo la Museveni kutaka kuwa kiongozi wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki? Lakini sasa baada ya kushindwa kwa azima hiyo ya kuundwa Shirikisho hilo sasa yaonekana amehamishia nguvu zake kwenye umoja wa Afrika na pengine akataka kuwa Rais au makamu wa Gadafi.

 

Ipo haja ya makusudi kabisa ya viongozi wa Afrika kuchekecha vizuri na kuzijua nia za watu hawa ambao wanasema kwamba hawawezi kungoka madarakani ila kwa mtutu wa bunduki halafu wanachochea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Afrika.

 

Lakini ikiwa lengo ni kuunganisha nguvu ili tufikie hatua ya kuendelea kiuchumi, kisiasa na kijamii, bado Afrika hatuna nguvu za kuunganisha, tunaunganisha nguvu zipi ikiwa watu wetu wanakufa kwa njaa? Ni nguvu zipi tunaziunganisha wakati bado mataifa kibao ya Afrika yanatafunwa na zimwi la vita za wenyewe kwa wenyewe? Au ni nguvu zipi tunaziunganisha ikiwa bado tunaoviongozi ambao wanasubiria kutoka madarakani kwa mtutu wa bunduki eti kwa kuwa waliingia kwa bunduki?

 

Ukweli ni kwamba Bara la Afrika linatawaliwa na mataifa yaliyoendelea kwa kiasi kikubwa sana, zipo baathi ya nchi ambazo pamoja na kujitapa kwamba zipo huru zinajivunia kujishabihisha na mataifa yaliyozitawala enzi za ukoloni kuliko ambavyo zinajishabihisha na mataifa ya Afrika.

 

Pia ni ukweli usiofichika kwamba mataifa ya Afrika yanaogopana, watu wanafanya mambo holelaholela lakini wanaonewa aibu, hata AU inaonekana kukosa uthubutu wa kuwaambia ukweli viongozi wa Afrika wanapopindisha sheria. Mtu anaiba kura anashauriwa akubali kuunda Serikali ya mseto kwa kuwa watu wanaogopa kumwambia ukweli wake. Hii ni ishara kwamba tungali na deni kubwa la kujiendeleza kidemokrasia ili tuweze kuunda United States of Africa yenye tija.

0 comments on 'United States of Africa' Kitendawili Kigumu

Add a comment

To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster

  • Type the words in the box below the image.

Email this blog post to a friend

To email posts to friends, you must be logged in. Login or Join Blogster

Friends

View All