Sumaye, ni toba ama ni kusahau?

May 16, 2008 / by saiboko

Hivi karibuni kulikuwa na mkutano wa pamoja kati ya wafanyabiashara wa Afrika na China uliofanyika kwenye hoteli maarufu ya Ngurdoto huko Mkoani Arusha. Mkutano huo ulikuwa ni fursa kwa wafanyabiasahara wa Tanzania na Afrika kwa ujumla kubadilishana mawazo na uzoefu wa kibiasahara na wenzao wa Taifa la China ambalo uchumi wake unakua kwa haraka sana.

 

Mh. F. Sumaye

 

Taifa la China linatajwa kuwa kwenye mataifa kumi ya Dunia ambayo uchumi wake unafanyavizuri sana. Ni kutokana na sifa hiyo hakuna ubishi kwamba fursa hiyo ilikuwa ni adimu na kama imetumika vizuri basi hakuna shaka kwamba kuna chanagamoto nyingi muhimu ambazo wafanyabiasahara wa Afrika wamezipata na ambazo ni muhimu kwa kukuza uchumi wa Afrika ambao bado unasuasua.

 

Kwenye mkutano huo wafanyabiasahara mbalimbali walipatanafasi ya kuzungumza na kubadilishana mawazo ikiwa kama njia ya kupeana changamoto. Miongoni mwa waliozungumza ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Frederick Sumaye. Vyombo vya habari vilimnukuu Sumaye akizungumza kwenye mkutano huo na kubwa alilolizungumzia lilikua ni kuwalaani wawekezaji kwa madai kwamba wanatuibia raslimali zetu? na ni kutokana na hilo ndio maana hatuendelei.

 

Maneno hayo ya Sumaye yanakuja ikiwa ni takribani miaka mitatu sasa tangu astaafu rasmi kutoka kwenye nafasi yake ya Uwaziri Mkuu aliyoishikilia kwa miaka kumi. Itakumbukwa pia kwamba ni kipindi chake alipokuwa Waziri Mkuu ambako Tanzania imeshuhudia kushamiri kwa ubinafsishaji wa mali za umma ambao pengine haujawahi kutokea kwa kipindi chote cha uhuru wa nchi hii? Ilifikia hatua mpaka baadhi ya Wananchi wakanong’ona wakidai kwamba nchi imeuzwa.

 

Lakini pia itakumbukwa kwamba huyu alikuwa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, utawala ambao kwa sasa unalalamikiwa vikali kwamba uligubikwa na zimwi la ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, nyingi ya fedha hizo zikiwa zinatokana na kusainiwa kwa mikataba lukuki ya ubinafsishaji, ndio leo hii tunasikia Serikali imefikia hatua ya kulazimika kuangalia uwezekano wa kumchunguza Mzee Mkapa baada ya kuona kwamba shutuma zinazidi kila uchao licha ya kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kuwataka Watanzania kumwacha Mzee Mkapa apumzike. Kitendo cha kung’ang’ania kwamba Mkapa na Mawaziri wake wachunguzwe ni ishara tu kwamba watu wanawasiwasi sana na jinsi mambo yalivyo kwenda wakati wa utawala wake.

 

Lakini kama tunakumbuka hata baada ya kustaafu Sumaye aliwahi kuhojiwa na akautetea utawala wa Mzee Mkapa na kusema kwamba ni utawala ambao ulifanikisha kuukuza uchumi wa Taifa la Tanzania kwa kiwango kizuri kabisa? Kama hivi ndivyo basi hakuna shaka kwamba kama lipo jambo kubwa lililofanywa na utawala wa Mkapa ni pamoja na ubinafsishaji wa mashirika ya umma na kuweka mazingira nafuu kabisa kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na misamaha mikubwa ya kodi kwa wawekezaji. Je sasa Sumaye anatuambia kwamba kazi hiyo haikuwa na manufaa kwa nchi ikiwa wawekezaji hawa ndio vinara wa wizi wa mali zetu?

 

Taarifa zimebainisha kwamba Sumaye kwenye hotuba aliyoitoa Ngurdoto alikiri kwamba alikuwa hajajua kwanini Tanzania na Afrika ni masikini mpaka alipokwenda kusomea shahada yake ya uzamili kwenye Chuo Kikuu cha Harvard. Hata hivyo ni vigumu kuyaamini maneno ya Sumaye kwa kuwa sio kweli kwamba kujua kwamba wawekezaji wanatunyonya kunahitaji mpaka mtu awe na shahada ya uzamili. Mbona wapo wananchi wengi tu wa taifa hili ambao walionya kuhusu ubinafsishaji na wakasisitiza kabisa kwamba madhara ni makubwa lakini bado Serikali ikaendelea na mipango yake? Je wakati huo Sumaye hakuwa anawasikia wananchi?

 

Taarifa zinasema kwamba Sumaye aliwahakikishia wafanyabiasahara wa Afrika na China kwamba Afrika ina rasilimali nyingi yakiwamo madini na mafuta lakini raslimali hizo hazijawahi kuvunwa kwa faida ya wazawa na badala yake yanafaidika mataifa yaliyoendelea pekee. Anasema kwamba madhali tunasafirisha malighafi badala ya bidhaa tusitegemee kabisa kuendelea. Maneno haya ni mazito na lau kama Sumaye angeyatambua wakati ule akiwa Waziri Mkuu na akayafanyia kazi tungekuwa mbali sasa. Wakati ule wananchi wakiambiwa kwamba ndege ya Rais na rada zitanunuliwa hata kama wananchi watakula nyasi, ulikuwa wakati muafaka wa kubadilisha matumizi na badala yake kujengwe viwanda ili tuachane na biashara ya kusafirisha malighafi, lakini badala yake Serikali ikaonelea ni bora ikanunue Rada na Ndege ya Rais kisha tuendelee kusafirisha malighafi.

 

Kwenye hotuba yake Sumaye alikiri kwamba licha ya kuongezeka kwa raslimali za Afrika bado Bara hili linashea ndogo kabisa kwenye soko la dunia ya 2.5% ambayo ni ndogo kuliko shea ya Taifa la China pekee. Hali hii inasikitisha na inadhihirisha hali nguma ya uchumi kwenye Bara la Afrika haswa ikizingatiwa kwamba Afrika inaandamwa na zimwi la ufisadi takribani kwenye mataifa yake yote.

 

Itakumbukwa kwamba hivi karibuni Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Addis Ababa alinukuliwa akisema kwamba matatizo ya Afrika hayawezi kufikia kikomo mpaka viongozi watakapo kubali kwamba utawala ni utumishi wa umma na sio sehemu ya kujinufaisha. Na huu ndio ukweli kwa kuwa viongozi wetu wanaubinafsi wa hali ya juu sana na kila anayepata nafasi anachumia tumbo tu, wasiofanya hivyo ni wachache ambao pia athari yao haiwezi kuonekana.

 

 Sumaye anatoa mfano wa jinsi ambavyo Tanzania imekuwa ikipoteza mapato kwa kusafirisha madini ambayo hayajasafishwa na kukatwa, anasema Tanzania ilikuwa inapata $100 kwa mwaka badala ya kupata $500 kwa mwaka. Lakini cha ajabu ni kwamba mbali na kujitambulisha kama mwanasiasa mtaafu hakutoa maelezo yeyote yanayoonyesha kwamba akiwa madarakani alijitahidi kuboresha hali ya mambo ili kufikia malengo ya $500 kwa mwaka. Ila anasema ikiwa madini hayo yangekatwa na kung’arishwa hapa nchini basi tungepata faida kubwa sana.

 

Lakini pia itakumbukwa kwamba mikataba ya madini iliyoingiwa wakati wa utawala wa Mzee Mkapa na Sumaye akiwa Waziri Mkuu imelipatia hasara kubwa Taifa hili, hasara ambayo itakuwa ngumu kufutika kwenye historia ya Taifa hili. Taarifa ya madini ambayo ilitolewa mapema mwaka huu inaonyesha kwamba, Tanzania imepoteza karibia Dola bilioni mbili za Kimarekani au asilimia arobaini ya bajeti yake ya mwaka mzima ikiwa ni hasara inayotokana na sera za madini zisizo na tija ambazo kwa kiasi kikubwa ziliwekwa na kusimamiwa na utwala wa Mkapa na Sumaye.

 

Pengine Sumaye amefikia pahala pa kujutia aliyoyatenda kwenye utawala wake na sasa anataka kutoa ushauri wa kujenga Tanzania mpya yenye manufaa kwa kila mwananchi baada ya kipindi kirefu cha wananchi kulalamika kwamba viongozi wanawatafuna.

 

Lakini pia kauli ya Sumaye imekuja wakati muafaka, wakati ambao Watanzania wanashuhudia mkondo mpya kwenye siasa za nchi yetu, wakati ambao mafisadi wanaitwa kwa majina yao halisi “fisadi”, wakati ambao vyombo vya habari vinaanza kuchangamka na kufanya kazi ipasavyo na kuachana na propaganda.

 

Ukweli ni kwamba ni bora anayekosea akajijua na akasoma alama za nyakati na kubadilika, kuliko wanaofumba macho na kujifanya kana kwamba hawaoni wakati nchi sasa inaanza kuamka kutoka kwenye lindi la adui ‘ujinga’. Hizi sio zama za kiongozi kuhojiwa kuhusu mali zake halafu akasema “acheni wivu wakijinga”.

 

Profesa Juma Mikidadi ambaye kwa sasa ni mhadhiri kwenye Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro aliwahi kusema kuwaambia wanafunzi wa chuo hicho kwamba lazima wabadilike na wajifunze kwenda kadri mabadiliko yanavyotokea, alisisitiza akisema kwamba mabadiliko yapo na kama mtu hataki kubadilika basi ajue yatambadilisha yeye.

 

Bila shaka Sumaye ameona mabadiliko na amekiri kwamba alikuwa hajui kwanini Tanzania na Afrika ni masikini, pengine ni kweli. Hata hivyo sijamhukumu.

 

0 comments on Sumaye, ni toba ama ni kusahau?

Add a comment

To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster

  • Type the words in the box below the image.

Email this blog post to a friend

To email posts to friends, you must be logged in. Login or Join Blogster

Friends

View All