Shamhuna na kauli za hatari

May 16, 2008 / by saiboko

Wahenga waliyanena kwamba “hakuna mapana yasiyo na ncha” na “hakuna marefu yasiyo na mwisho”, misemo hii imemfanya mwanadamu aishi kwa matumaini siku zote kwa kuamini kwamba ipo siku atayavuka mabonde na milima ya shida na taabu na hatimaye afike anapopataka. Pia tukirudi kwenye dini, zote zinasisitiza subira, kwa anaye amini subira inavuta heri.

 

Ramani ya Visiwa vya Zanzibar na Pemba

 

Watanzania kama walivyo binadamu wengine nasi tu miongoni mwa wanaosubiri kwa kuwa licha ya ugumu wa maisha yetu kuzidi bado hatujakata tamaa, bado tunaamini kwamba ipo siku tutayavuka yote haya. Ndio maana bado nchi yetu ingali na amani kuliko nyingine zote Afrika, japo wanasema kwamba kwenye njaa hakuna amani bado sisi tunaamini kwamba sio lazima tutumie ncha ya upanga, ndio maana kila siku tunasisitiza demokrasia ichukue mkondo wake kwenye masuala mazito na tete ambayo yasipo pewa uzito na umakini unaopasa yanaweza kutupeleka pabaya.

 

Lakini pia inafahamika vizuri kabisa kwamba kwenye msafara wa Mamba, Kenge wamo na hivyo ndivyo ilivyokuwa hata enzi za Mitume, wanafiki wapo kwa zama zote. Hawa ni watu wasio weza kuweka ahadi na kuitimiza, ni watu ambao kila watakapokaa na wenzao wakaafikiana juu ya jambo basi wao watakubali lakini ipo siku watabadilika kama vinyonga, ni watu ambao hawana ujasiri wakusema ukweli wao kama wasemavyo wazungu “speak your heart” wao kamwe hawana ujasiri wa kuzungumza yaliyopo ndani ya nyoyo zao ila ni mashuhuri wa kuzungumzia vipembeni.

 

Ukweli ni kwamba tabia kama hizi haswa zinapowanyemelea viongozi wakubwa wa kitaifa inakua ni hatari kwa kuwa ule msemo wa subira waweza kushindwa na ule wa “ngoja ngoja yaumiza matumbo” wananchi watachoka kusikiliza lugha gongana za wakuu wao na badala yake watahisi wanachezwa shere na matokeo yake ni mabaya sana. Ndio maana kwenye kundi la watu lazima kuwe na kiongozi, kiongozi ndiye mwenye mamlaka ya kutoa msimamo wa kundi la watu badala ya kuwa tayari wamekubaliana na wala sio kila mtu kujisemea ovyoovyo.

 

Kwa uzoefu wa matukio yanayoendelea nchini kwa siku hizi za karibuni, inaonekana kabisa kwamba viongozi wetu wanakosa nidhamu ya kiutendaji. Kwenye taaluma ya Mahusiano ya Uma (Public Relations) tunajifunza kwamba kila linapotokea janga au tatizo lolote kwenye uongozi lazima kuteuliwe msemaji mkuu, pia kuwe na ufuatiliaji kwamba huyo anayesema habadilishi maneno kutoka yale yaliyokubaliwa na menejimenti na kuingiza yakwake. Hili ndilo jambo ambalo pengine viongozi wetu wanashindwa kulifanyia kazi ipasavyo.

 

Kwenye sakata la Muafaka wa kisiasa Zanzibar ndipo tunakopata mfano mzuri wa mvurugano uliopo kwa viongozi wetu, hii inatokana na ukweli kwamba kila mtu anafikiri kwamba anaweza kuzungumzia masuala ya muafaka bila kujua kwamba yeye ni kiongozi na maneno yake kwa wananchi yana mshindo mkuu. Matokeo yake maneno ya mtu mmoja yanchukuliwa kuwa ni msimamo wa Serikali au chama fulani wakati pengine ni maneno ya mtu binafsi.

 

Sote tunafahamu kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) kilishakutana Butiama kikatoa maathimia yake kuhusu suala la muafaka Zanzibar, kama tunapinga maamuzi ya NEC-CCM au tunayakubali, hiyo sio mada yangu kwa leo ila najaribu tu kuvuta taswira ya azimio la Butiama ili niweze kuiweka vizuri mada yangu.

 

Kimsingi Watanzania wote wanaamini kwamba kilichofikiwa Butiama ndio kauli ya CCM nzima kwa kuwa mpaka sasa mbali ya madai kwamba kuna makundi ndani ya chama hicho kikongwe nchini hakuna kundi hata moja lililojitenga waziwazi, isitoshe Katibu Mkuu wa CCM, Mzee Yusufu Makamba alishakanusha uvumi huo. Hivyo basi tungali na imani kwamba CCM ni moja na  kwa vyovyote vile kauli yake ni kauli ya wote kwenye chama. Lakini pengine kwa kukosa kulitambua hili ama kwa ujeuri, wapo viongozi ndani ya chama hicho ambao wanataka kucheza na amani ya nchi yetu kwa maslahi wanayoyajua wenyewe.

 

Kauli iliyotolewa na Naibu Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Ali Juma Shamhuna juu ya Muafaka Zanzibar ni katika mambo ambayo yanakishushia hadhi chama cha mapinduzi na kukifanya kionekane kwamba hakina kauli moja yenye nguvu. Katiaka hali ya kawaida Shamhuna hakutakiwa kutoa kauli ya kudai kwamba hakutakuwa na Serikali ya Mseto Zanzibar na kumtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad asahau ndoto yake hiyo kwa kisingizio cha kwamba katiba haimpi nafasi hiyo kwa kuwa yeye sio miongoni mwa viongozi wa Baraza la Wawakilishi.

 

Shamhuna anadai kwamba Dunia ya leo sio ya kulazimishana, bila shaka hajakosea hata kidogo kwa kuwa tumo kwenye ulimwengu ambao Demokrasia inaheshimika sana, lakini hajafafanua vizuri ni nani anamlazimisha nani? Je alilazimishwa na NEC-CCM kukubaliana na maadhimio? Je akiwa kama mjumbe wa NEC-CCM na ambaye pia alihudhuria mkutano wa Butiama alishindwa vipi kutoa kauli yake kwenye mkutano ili ijadiliwe? Huu ni usaliti kwa kuwa kama kiongozi anakua na dukuduku lake halafu anashindwa kulisema kwenye mikutano na viongozi wenzake na anakwenda kusemea huko pembeni ni ishara tu kwamba hajiamini.

 

Anaposema kwamba hizi sio zama za kuburuzana anatakiwa ajue pia kwamba Demokrasia inasisitiza utawala wa wengi na haki kwa walio wachache, hivyo basi hata kama wahafidhina wa Zanzibar wangekataa maadhimio ya chama chao na ikatokea kwamba wao ni wachache bado demokrasia ingewapendelea waliowengi na wala huku sio kuburuzana bali ndivyo inavyotakiwa. WanaCCM wa Zanzibar wenye mawazo kama ya Shamhuna wanajidanganya kwa kuwa kama wapo ndani ya CCM wao wanatakiwa kufuata maamuzi ya chama chao ama la sivyo watuambie kwamba hawana imani na viongozi wao wakuu au wajitenge. Huu ndio ukweli hata kama unauma.

 

Ndio maana alipotoa kauli ya chama dhidi ya maneno ya Shamhuna, Katibu wa Itifaki na Uenezi wa CCM Taifa, Kapteni John Chiligati aliweka bayana kwamba kauli aliyoitoa Shamhuna ni ya kwake mwenyewe, Chiligati alisema kwamba CCM inatambua maamuzi ya NEC kuwa ndiyo ya juu kabisa na ndio msimamo wa chama kwa hiyo Shamhuna hawezi kukisemea chama. Kwa hili CCM wameonyesha ukomavu wao kwenye masuala ya uongozi kwa kuwa ndivyo inavyotakiwa kwamba kama atatokea mtu akaropoka kwenye chama ama kampuni basi njia pekee ni kumkanusha ili chama ama kampuni liendelee kuonekana safi mbele ya macho ya watu. Hii kitaalamu inaitwa (Damage Control au Crisis Management)

 

Hata hivyo Chiligati alinukuliwa akisema kwamba NEC-CCM wakiwa Butiama kimsingi walikubali mapendekezo yote lakini walibaini baadhi ya mapungufu na kuiagiza kamati ya mazungumzo ya CCM ikutane na ile ya CUF ili wafanye marekebisho. Lakini pia itakumbukwa kwamba CUF ilishatoa msimamo wake kwamba haitaendelea tena na mazungumzo na kumtaka Rais Kikwete awakutanishe Maalim Seif na Rais Amani Karume ili wayamalize kwa kuwa msimamo ulikua kwamba saini za Makamba na Maalim Seif hazitoshi.

 

Hata hivyo mbali na Shamhuna kudai kwamba aliitwa kwenye jimbo lake la Donge kwenda kuongea na Wazee juu ya suala zima la Muafaka, baadhi ya viongozi wa CUF wamekanusha madai hayo huku wakisema kwamba Shamhuna alifanya hivyo makusudi kabisa ili afikishe dukuduku lake na ili aweze kuchochea chuki na vurugu miongoni mwa Wazanzibar.

 

Itakumbukwa kwamba nimewahi kuandika makala kuzungumzia azimio la Butiama ambalo mimi nilihisi kwamba limetuacha solemba kwa kuwa tulikuwa na matarajio ya juu sana na kumbe hakukuwa na maamuzi ya kutisha. Lakini kwenye makala ile niligusia hotuba aliyokuwa imetolewa na Shamhuna alipowasili huko kwa ajili ya mkutano, Shamhuna alionyesha waziwazi chuku aliyonayo juu ya Maalim Seif na chama chake cha CUF. Kwa kauli za kusema kwamba CUF wanataka sifa tu kwa kuwarubuni wananchi kwamba wanaweza kuongoza nchi ili hali hawana uwezo huo, inakua rahisi kwa mwananchi yeyote kuamini kwamba Shamhuna anaweza kufanya chochote kuvuruga Muafaka wa Zanzibar.

 

Lakini pia mtu kama huyu ni bora akaitwa na kamati ya maadili akahojiwa kwa kuwa pengine kuna anachokifahamu au pengine yeye ni kama mdomo wa wenzake na kwa mantiki hiyo kauli yake ni kauli ya wenzake wote wa Zanzibar. Nasema hivi nikizingatia kauli ya Shamhuna aliyoitoa na kudai kwamba kama wapo watakaosema kwamba anachafua hewa ya kisiasa na wakamwajibisha kwa hilo, yeye atarudi kwa wananchi wake waliomchagua akafanye nao kazi. Kazi gani? Hakusema. Kufikia hatua ya kutamani au kuridhia kuachia madaraka kwa kile unachokiamini kwamba ni sahihi ni hatua ya juu sana ya imani, ni ishara kwamba kuna jambo ambalo Shamhuna analiona kwamba linaenda kinyume kabisa na ndio maana upo umuhimu wa mtu huyu kuhojiwa ili atoe ukweli wa mambo.

 

Ukweli ni kwamba kama kauli ya Shamhuna ni msimamo wa viongozi wote wa CCM Zanzibr, basi ipo kazi kwa CCM kuweza kulipatia ufumbuzi wa kudumu tatizo la Zanzibar.

0 comments on Shamhuna na kauli za hatari

Add a comment

To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster

  • Type the words in the box below the image.

Email this blog post to a friend

To email posts to friends, you must be logged in. Login or Join Blogster

Friends

View All