Serikali iliwatelekeza Wajasiriamali Sullivan

June 19, 2008 / by saiboko

Mkutano wa nane wa Leon H. Sullivan umemamalizika hivi karibuni huko Arusha. Ni mkutano wa kihistoria ambo watanzania waliusubiri kwa muda mrefu huku Serikali yao ikihaha huku na kule katika harakati zakuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa ilimradi tusitie aibu. Katika mambo yaliyochukuliwa kipaumbele ilikuwa ni pamoja na ulinzi mzito kiasi cha kuwafanya wananchi walalamike kwa kuwa walijihisi wananyanyaswa haswa ikizingatiwa kwamba wahanga wa makosa ya uzururaji walikithiri.

 

Zaidi kilichowafanya Watanzania kuwa na hamu kubwa ya mkutano huo ni zile mbiu za Serikali ambazo ziliwahakikishia wakazi wa Arusha na watanzani kwa ujumla kwamba mkutano huo ungeleta neema ya aina yake kwa Taifa letu. Kwamba ungechangia kukua kwa uchumi wetu kwa kuwa vivutio mbalimbali vya utalii vingetangazwa kwa wageni. Lakini  kwa mtanzania mmoja mmoja haswa wajasiriamali waliambiwa kwamba mkutano huo ungewajengea fursa nzuri sana ya kuuza mali zao kwa wageni hao na hivyo basi wangejivunia mapesa kibao.

 

Itakumbukwa kwamba mara baada ya kusema hivyo Serikali ilihakikisha pia kwamba inawahamasisha wajasiriamali wengi ipasavyo ili waweke kambi Arusha wasubirie madola ya Wamareka weusi wenzetu waje wawaletee neema. Hata hivyo wajasiriamali hao baada ya kuhakikishiwa kwamba nao watapangwa kwenye ratiba ya mkutano huo ili wageni wapate nafasi ya kuwatembelea, ndipo walipoamua kwamba wajizatiti ili waweze kuwarizisha wateja wao pindi watakapo kwenda kuwatembelea.

 

Taarifa zinasema kwamba wajasiriamali kutoka Mikoa 17 ya Tanzania walimiminika kwenye mji huo wa kitalii wa Arusha pamoja na wenzao kutoka nchi za jirani ikiwamo Kenya. Hawa walikuwa na bidhaa za kila aina ili kuhakikisha kwamba wanawavutia wateja wao, wengine walitengeneza bidhaa zenye nembo ya Sullivan mahususi kwa wageni wao. Hata hivyo cha ajabu ni kwamba hakuna mgeni wa mkutano huo aliyetembelea maonyesho hayo yaliyokuwa yameandaliwa katika viwanja vya nanenane nje kidogo ya mji wa Arusha.

Kutokana na hali hiyo wajasiriamali hao wamelalamika sana huku wakiielekezea serikali lawama kwa kile wanachodai kama ulaghai wa viongozi wa Serikali. Wajasiriamali hawa wanasema kwamba ulaghai  huo umewapelekea kupata hasara kubwa sana kwa kuwa wametumia pesa nyingi kununua bidhaa ambazo kimsingi hazikuuzika, kama haitoshi vile wanadai kwamba walikuwa wanalipia 75,000/= kila siku kama gharama za kupangisha mabanda ya nanenane.

 

Kimsingi wajasirimali hawa wamezulumiwa na Serikali kiasi cha kukosa kabisa imani na viongozi wao. Hii inatokana na ukweli kwamba tumeshuhudia kilichomkuta Waziri wa viwanda biasahara na masoko Dk. Mary Nagu alipowatembelea wajasiriamali hao, nusura wamtoe macho kwa hasira. Inasemekana kwamba Waziri huyo alikwenda kwenye mabanda hayo kuwasihi wajasiriamali hao wasiandamane kwa kuwa zilikuwapo tetesi kwamba wangefanya hivyo kuonyesha hisia zao.

 

Dk. Nagu yaonekana alishinda kuzisoma alama za nyakati na akajikuta akitinga kwenye kundi la wajasiriamali wenye hasira huku akiwa na tabasamu kana kwamba alikuwa anazungumza na  watu wenye furaha, hivi wangeitoa wapi furaha wenzetu wale? Furaha ya kutelekezwa huku wakilipia mapesa kibao bila kujua hatma yao? Hii ni aibu kubwa na imeonyesha jinsi ambavyo tunawathamini wageni kuliko wenzetu. Hivi kweli twaweza kuwaalika wajasiriamali wa Marekani na kuwatelekeza? Je ni vipi tutaukuza uchumi wa watu wetu na kuwaletea maisha bora ikiwa tunaweza kuwafanya vile?

 

Mataifa yote yaliyoendelea yanawathamini sana wafanyakazi na wafanyabiasahra kwa kuwa wanamchango wao mkubwa kwa pato la taifa. Hivi majuzi tumeshuhudia ujio wa mwanamuziki maarufu wa Marekani anayefahamika kwa jina la kisanii kama senti hamsini (50 Cent). Kinachoshangaza ni kwamba 50 Cent alikuja na jopo la watu wengi sana wakiwamo makachero wa Marekani waliotumwa kuja kuhakikisha kwamba anarudi salama ili aendelee kulipatia taifa lake faida inayotokana na kodi anayoilipa. Lakini kwa Tanzania anaweza kusafiri mfanyabiasahara maarufu sana na hakuna anayehangaika kujua anakwenda vipi na usalama wake ukoje. Hili ni jambo la kusikitisha.

 

Wajasiriamali waliotelekezwa Arusha wanaapa kwamba kamwe hawahudhuria tena maonyesho yaliyoandaliwa na Serikali, wengine wanafikiria hata kususia maonyesho ya sabasaba na nanenane. Kwa madai haya watanzania pengine tusione uzito wa jambo lenyewe, lakini ukweli ni kwamba matamshi kama haya kutoka kwenye vinjwa vya wajasiriamali waliotoka Mikoa 17 nchini na wengine nchi za jirani, ni mazito sana. Pia ni vyema ikakumbukwa kwamba wajasiriamali hawa wanavyama vyao ambavyo vipo kwa ajili ya kuwasaidia wanachama wao haswa kwenye matatizo kama haya.

 

Kutokana na ukweli huo ipo hatari kwamba jambo hili likichukuliwa kimzahamzaha wajasiriamali hawa kwa msaada wa vyama vyao wanaweza kutoa tamko la kugoma kushiriki maonyesho yoyote yajayo. Je ikiwa hivyo tutamudu kufanya maonyesho bila kuwatumia wazawa? Tutaonyesha nini? Nasema haya nikizingatia kwamba tayari Chama cha Maonyesho na Kilimo Tanzania (TASO) kupitia katibu wake mkuu Peter Ngassa kimeunda kamati maalumu kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao kwa Rais Jakaya M. Kikwete. Ninamna gani Rais atajibu? Hapa ndipo kutapelekea kutangamaa au kuharibika kabisa kwa hali ya mambo. Bila shaka Kikwete atatumia busara katika jambo hili.

 

Mjasiriamali mmoja wa Kenya aliyenukuliwa na gazeti moja la kila siku la hapa Tanzania analaani kitendo cha kuachwa solemba na Serikali ya Tanzania, anasema kamwe hatakuja tena kwenye maonyesho yaliyoandaliwa na Serikali na kubwa zaidi analalamikia fedha zake zilizopotea bila faida, anadai kwamba alitakiwa kulipa Dola za Marekani 4,000 kama ada ya kushiriki maonyesho hayo ukiachia mbali 75,000/= alizokuwa analipa kila siku na mwisho wa siku hakupata kitu anasema ni bora wahusika wakapima kwa nafasi yao na wakamrudishia gharama zake. Kimsingi kitendo hiki hakina tofauti sana na wizi kwa kuwa kumwibia mtu ni kumzulumu mali yake na hichi ndicho kilichotokea Arusha.

 

Wakati wajumbe wa mkutano wa Sullivan wanazungumzia umuhi mu wa kupendana kama waafrika na kusaidiana kwa hali na mali wajasiriamali wetu walikuwa wanapiga miyayo  huko nanenane  wakiwa na matumaini ya kifaranga kwamba watanyonya kesho, mpaka mkutano unamalizika wajumbe wanasherehekea wakigonga cheers kwa mafanikio lukuki yaliyopatikana, wajasiriamali wetu walikuwa wanafungasha virago wakiwa wamejawa na huzuni kutokana na hela  zao walizoteketeza bila mafanikio.

 

Suala la kustaabisha ni kwamba kumbe wakati wale wajasiriamali wakiwa wanasubiria kule kwenye viwanja vya nanenane, huko kwenye viwanja vya ukumbi wa mikutano wa kimataifa (AICC) kulikuwa kumeandaliwa maonyesho mengine ambayo yalitembelewa na wageni wa mkutano wa Sullivan. Wananchi wengi bado wanajiuliza kulikoni maonyesho yaandaliwe sehemu mbili halafu mengine yatembelewe na mengine yatelekezwe? Waandaaji hawaoni kama wamekosea kuandaa maonyesho sehemu mbili tofauti? Ukweli ni kwamba ikiwa bidhaa za AICC na za nanenane zilikuwa zinafanana basi hakukua na haja ya kuweka sehemu mbili za maonyesho.

 

Iliripotiwa kwamba kwenye maonyesho hayo ya AICC Rais Kikwete aliiagiza wizara ya viwanda, biasahara na masoko kuhakikisha kwamba wachonga vinjago wanapatiwa maeneo ya kudumu kama ilivyo pale Mwenge Jijini Dar es Salaam. Lakini cha ajabu ni kwamba hakukua na mwakilishi wa Wizara wakumwambia Rais kwamba wajasiriamali wengine walikuwapo kule kwenye viwanja vya nanenane nao wakiwa wanasubiria kutembelewa. Hebu tujiulize nini kiliwakwamisha wageni wa Sullivan kushindwa kwenda nanenane? Lazima tujiulize kwa kuwa tunaambiwa kwamba ulinzi uliimarishwa asilimia mia, barabara zilikarabatiwa, Arusha ilikuwa inangara kila kitu safi, kumbe tatizo nini?

 

Dhana ya utumishi wa umma haiwezi kufikiwa kama bado Mawaziri wetu wanakubali kuzomewa na bado wakalala usingizi usiku, siku zinapita na wala hawaoni kama kuna tatizo, kwanini hata usiombe radhi? Au ndio kusema kwamba mkubwa hakosei? Sawa hata kama hivyo ndivyo lakini pia mkubwa huteleza na ikiwa kuteleza sio kuanguka basi tunatarajia kwamba kulikuwa na kila haja ya kulisafisha jina la Serikali mapema kabisa kabla hayajafika kwa Jumbe. Ukweli ni kwamba kukimbia tatizo hakuwe kulimaliza bali kutalikuza zaidi kwa hiyo ipo haja ya kulishughulikia suala hili na kuhakikisha kwamba halitokei tena.

 

Suala hili inabidi liundiwe tume ya uchunguzi ili ikigundulika kwamba waandaaji walikuwa na nia mbaya basi wawajibishwe na ipo haja ya kuwarudishia fedha zao wajasiriamali waliotelekezwa kwenye viwanja vya nanenane.

 

 

 

 

0 comments on Serikali iliwatelekeza Wajasiriamali Sullivan

Add a comment

To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster

  • Type the words in the box below the image.

Email this blog post to a friend

To email posts to friends, you must be logged in. Login or Join Blogster

Friends

View All