Nchi zilizoendelea Duniani kote zinamambo kadhaa ambayo kwayo zinajivunia kwamba zimeendelea, ni mjumuisho wa mambo mengi sana katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ndio kusema kwamba wanaposema demokrasia basi wanahakikisha kwamba inatekelezwa kwa kiwango cha juu kabisa na wanapozungumzia suala la huduma za jamii wanajitahidi kuhakikisha kwamba zinapatikana katika viwango ambavyo vinarizisha kabisa.

Waziri wa Miundombinu Mh. Andrew Chenge
Sifa hizo kwa nchi zinazoendelea Tanzania ikiwemo zinakuwa kinyume hashwa zikichangiwa na kuwepo kwa hali mbaya ya kiuchumi, ukame, vita na majanga mengine mengi. Wapo wanaodai ya kwamba bado sisi katika baadhi ya sekta tuko nyuma kuliko walikokuwa Waingereza miaka ya 1700’s, hii yawezekana ni kweli kwa kuwa vielelezo vipo. Lakini pia inakatisha tamaa kwani kama ikiwa hivyo ndivyo basi kuna kila dalili kwamba sisi pengine tusifike kabisa kwenye hatua ya kuitwa nchi ileyoendelea milele.
Tunapoitupia ukope nchi yetu kwa mfano tunaona kuna mapungufu mengi ya kiutendaji ambayo tayari Serikali imeanza kuyashughulikia, lakini bado kasi iliyopo ni ndogo na ukweli ni kwamba matatizo haya ya kiutendaji haswa kwenye utumishi wa umma yanaipeleka pabaya nchi na mustakbali wa wananchi kwa ujumla.
Suala ambalo hivi karibuni limekuwa likifukuta ni suala zima la mikataba mibovu ambayo viongozi wetu haswa Mawaziri wa Wizara mbalimbali kwa nafasi zao wanaisaini bila kuzingatia maslahi ya mikataba husika kwa wananchi na Serikali kwa ujumla. Mikataba kama Richmond, IPTL na mingineyo mingi imeshalalamikiwa vya kutosha kabisa na hivi karibuni tumeshuhudia baadhi ya Mawaziri wakiwajibika kwa kutuhumiwa kushiriki katika kusaini mkataba wa Richmond ambao uchunguzi uligundua kwamba haukuzingatia maslahi ya Taifa.
Wakati tunazungumzia suala la Richmond, limeibuka jengine la Shirika la Reli Nchini (TRL) ambalo zamani likijulikana kama TRC, imeripotiwa na vyombo kadhaa vya habari nchini kwamba mkataba kati ya Serikali na Kampuni ya Reli ya India (Rites) wa kukodisha injini 25 za treni ni kitanzi chengine kwa Serikali ya Tanzania kama kilivyo kile cha Richmond na vinginevyo. Mgogoro kwenye mkataba huo nao unazungumziwa kuwa unatokana na masharti magumu ambayo yamo kwenye mkataba huo na ambayo kwa kiasi kikubwa yanaibana Serikali.
Mkataba huo wa miaka mitano na ambao ni mpya kabisa unasemekana kwamba unaitia Serikali kitanzi kwa kuwa kama ule wa Richmond, huu noa unaitaka serikali kulipia gharama zoto za matengenezo iwapo injini hizo zitaharibika zikiwa kazini, gharama hizo zinajumuisha pia gharama za kuzisafirisha injini hizo kupelekwa India kwa matengenezo kama itabidi kufanya hivyo kwa kushindwa kuzitengenezea hapa Tanzania.
“Mkataba huo umekadiria gharama za kusafirisha injini moja ya treni kutoka Tanzania hadi India kuwa ni dola za Marekani 35,000 sawa na Sh. 41 milioni na gharama za kusafirisha injini zote 25 kwenda India ni dola za Marekani 1,435,000 sawa na Sh. 1,025,000,000.” Ilisema moja ya habari juu ya mkataba huo.
Hiki ni kiwango kikubwa haswa ikizingatiwa kwamba mkodishaji ambaye hapa ni Serikali atalazimika kusafirisha injini zote 25 kurudisha India mara baada ya mkataba kuisha. Hizi ni gharama ambazo hazikuwa na msingi wowote wa kuwapo kwa kuwa ni suala la kujiongezea matatizo kwenye Taifa kama hili ambalo tayari linamatatizo lukuki ya kutatua.
Hata hivyo kinachoshangaza zaidi ni kwamba kama ulivyokuwa mkataba wa Richmond ambao ulikuwa unalitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kulipia gharama zote za uendeshaji zikiwapo za kununua vipuri na kuvisafirisha kuja nchini, huu wa TRL nao unailazimu Serikali kufanya hivyo tena kwa masharti kwamba Rites ndio watakuwa wasambazaji pekee wa vipuri hivyo. Hiki ni kitendawili kingine cha mikataba mibovu ambayo kwa karne hizi haipaswi kuwapo, suala zima la kufaidika kwa pande mbili “win- win situation” hapa halifikiwi.
Suala linaloshangaza zaidi ni kwamba baadhi ya wafanyakazi wa TRL waliohojiwa wamethibitisha kabisa kwamba injini hizo za kukodi zinauwezo mdogo sana wa kufanya kazi kiasi ambacho kinaiweka sekta hiyo kwenye matatizo ya kukwama kwa treni mara kwa mara. Wanasema kwamba injini hizo haziwezi kusafiri kutoka Dar es salaam kwenda Mikoa ya mbali kama Mwanza na Kigoma na kama zikifanya hivyo matatizo kadhaa yanatokea ikiwamo kukwama kwa treni njiani. Wanasema kwamba wakati zile zilizokodishwa na TRC mwaka 1997 zilikuwa na uwezo wa 80 class, hizi za rites zina 73 class. Hii ni ishara tosha kwamba kunaukosefu wa umakini kwa kuwa kinachohitajika ni kupiga hatua mbele na suala la kukodi injini zenye uwezo mdogo kuliko zilizokuwapo awali linalengo la kuturudisha nyuma kimaendeleo.
Wenzetu kwenye nchi zilizoendelea kila siku wanajitahidi kuhakikisha kwamba wanafanya mambo makubwa zaidi ya pale walipo sasa ili kujiwekea uhakika wa ushindani kwenye nyanja za kiuchumi, kiasa na kijamii, wakati huo sisi ndio kwanza tunaingia mikataba isiyo na tija, mambo kama haya yanasababisha tunyosheane vidole kila uchao, japo tunaambiwa kwenye vitabu vya dini kwamba kabla hujasimama kusema aibu za mwenzako, utizame za kwako kwanza, lakini kwenye hili hatuna budi kuzitizama na kuzinyoshea aibu kama hizi vidole kwa kuwa zinakusudia kuliangamiza taifa.
Wapo wanaodai kwamba ni kweli mkataba huo unamapungufu yake lakini hauwezi kuibana Serikali kwa kuwa ulisimamiwa na maafisa wa Serikali mpaka mwisho, hoja hii ingekuwa na msingi hapa kama tungekuwa na viongozi waaminifu na wenye uzalendo kwa nchi yao. Tunaposema hivi ni sawa na kufumba macho, hii inatokana na ukweli kwamba hata mikataba kama Richmond na IPTL ilisimamiwa na haohao viongozo wa Serikali lakini sifa hiyo haijaifanya mikataba hiyo kuwa na manufaa makubwa kwa Serikali zaidi ya kuwa kitanzi kinachotaka kuliangamiza shirika letu pekee la umeme nchini na kulifanya liendeshe biashara kwa hasara kubwa na hivyo kulazimika kuhamishia machungu yake yote kwenye kodi kwa mlaji ambaye ni mwananchi wa kawida na hivyo kuzidisha ugumu wa maisha kwa wananchi.
Alipoteuliwa tena kuwa Waziri wa Miundombinu Mheshimiwa Andrew Chenge alipata ukinzani kutoka kwenye vyombo vya habari kadhaa nchini na kwa wananchi kwa ujumla wakidai kwamba hakustahiki kurejeshwa kwenye baraza la Mawaziri, tena kwenye Wizara nyeti kama hii ya Miundombinu. Wakati ule kulikuwa na minong’ono juu ya matatizo kadhaa ya kiutendaji ndani ya Wizara hiyo, wapo waliolalamikia sana suala la ujenzi wa Barabara ya Samnujoma pale Dar es salaam kuchukua muda mrefu kuliko ilivyokuwa imepangwa wakati mradi huo ulipoanza. Lakini wengine walikwenda mbali zaidi na kuugusia mkataba huu kati ya Serikali na Rites na wakadai kabisa kwamba hauna maslahi kwa nchi.
Ukweli ni kwamba kwenye nchi zilizoendelea usafiri wa treni ni usafiri muhimu sana, ndio usafiri wa haraka wa pili baada ya ule wa ndege na hii inatokana na ukweli kwamba wao wamepiga hatua kubwa kwenye teknolojia hiyo na sasa wanatumia treni za umeme ambazo zinatembea kwa kasi zaidi. Lakini wakati wenzetu wanafikia hapo kwenye ubora wa hali ya juu kabisa sisi bado tunakodisha injini za kizamani zaidi ambazo zimepitwa na wakati kana kwamba hatuhitajii maendeleo haya yaje kwetu. Tumekosa kabisa wivu wa maendeleo na tunashindwa kuendelea kwa sababu hiyo, kwa mfano wakati wenzetu wanajenga barabara za kupita juu na chini ya aridhi, sisi mpaka leo tumeshindwa hata kujenga daraja la kuiunganisha Kiganboni na Sehemu nyingine za Jiji la Dar es salaam, tumeshindwa hata kuboresha usafiri wa pale kivukoni matokeo yake tunacheza kamari na maisha ya watu.
Wakati mwingine Serikali inashindwa hata kusimamia baadhi ya mambo kutokana na kasoro ambazo zipo kwenye Serikali yenyewe. Kwa mfano Serikali inaweza vipi kuwasimamia wafanyabiashara ambao wanamiliki vyombo vya usafiri ikiwa yenyewe haiwezi kuwa na vyombo vyake bora vya usafiri? Treni ndio hizo hazieleweki wala haziaminiki kwa safari, zipo tu bora liende, vivuko na meli za Serikali nazo zipo mahututi. Itakumbukwa kwamba kuna kipindi kulitolewa kauli kwamba malori yote yaliyojengewa bodi za mabasi yangesimamishwa maramoja kwa kuwa ni hatari kwa usalama wa raia. Lakini wakati huo huo Serikali inamiliki treni ambazo humo ndani ukiingia ni kama mahabusu na injini zake ndio hizo zinautata na hapo tumeingia mkataba na kampuni ya kigeni ili kuboresha huduma, sasa utajiuliza hapa nani anaweza kumsimamia mwenzake wakati sekta binafsi na serikali wote ni hawajiwezi?
Suala la mikataba yote kupitiwa upya kama walivyoshauri baadhi ya wabunge na wachambuzi mbali mbali linabakia kuwa la msingi sana hashwa ikiwa kweli tunataka maendeleo endelevu. Pia ni muhimu kuangalia umuhimu wa kuendelea na mikataba hii ambayo ina utata na ikiwezekana ni bora tukaiepuka kabisa.
0 comments on Mikataba mibovu na ukosefu wa kiu ya maendeleo
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster









