Makala hii ilichapishwa kwenye gazeti la Rai Tarehe 12/07/2007
Jengo la Bunge Dodoma
Wanadamu tunamipango mingi ya maisha, mingine tunaipanga tukiwa na uhakika na uwezo wa kuitekeleza na baadhi tunaipanga bila hata ya kujua ni kwa namna gani itatekelezeka. Wakati mwingine hata baada ya kugundua kwamba mipango yetu haitafanikiwa tunashindwa kuikanusha na kufikiria mipango mbadala.
Lakini hata hivyo wahenga wetu walishatutanabahisha ya kwamba kunena ni ada ya mja, lakini wakaendelea kusema kwamba muungwana hutenda. Japo tunasema kwamba hakuna lisilo wezekana, lakini bado tunakubaliana kwamba kuna baadhi ya mambo ambayo hayawezekani kutokana na hali halisi ya maisha ya mtu, watu ama taifa kwa ujumla.
Pia katika maisha kunavitu ambavyo ni muhimu ili mtu aweze kuishi. Vitu kama nyumba, chakula na malazi ni muhimu kwa kila mtu. Lakini kwa upande wa nchi kuna vitu ambavyo ni muhimu na vingine ni vya ziada kwa maana kwamba viwepo au visiwepo nchi itaendelea kua na hali nzuri na wananchi wake wataishi kwenye amani na uhuru.
Ni miaka ishirini na nane sasa imepita tangu Serikali ya Tanzania itangaze adhima yake ya kuufanya Mkoa wa Dodoma uwe makao makuu ya serikali. Wakongwe wa siasa za Tanzania wanadai kwamba wakati ule ilipotangazwa adhima hiyo, serikali ilisema kwamba litakua ni jukumu lake kuhakikisha kwamba makao hayo makuu yanakua ya kweli.
Lakini kama ilivyo ada ya mja kunena, bado ndoto hiyo haijatekelezeka, sio kwa maana kwamba haiwezekani lakini mazingira ya Dodoma bado hayajaweza kukidhi mahitaji ya serikali na taasisi zake.
Hata hivyo hivi karibuni kumekua na mijadala Bungeni juu ya suala hilo la kuifanya Dodoma kua makao makuu. Cha kushangaza ni kwamba bado Serikali inatetea mipango hiyo na kudai kwamba iko mbioni kukamilika.
Kwenye kipindi maarufu kinacho endeshwa na televisheni moja hapa nchini juu ya shughuli za Bunge kwa wiki nzima, kulikua na mdahalo wa kujadili mambo yaliyojiri Bungeni wiki ile. Mwendesha kipindi aliwauliza Mawaziri waliokua wamealikwa kwenye kipindi juu ya msimamo wa Serikali kwenye adhima hiyo ya kuifanya Dodoma kua makao makuu ya serikali.
Mawaziri wanasema mipango hiyo bado ipo na inachukuliwa hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa mfano waziri wa TAMISEM Bw. Mizengo Pinda yeye alisema Wizara yake tayari ina ofisi Dodoma na anatarajia nyingine pia zitafanya hivyo.
Hata hivyo mwendesha kipindi alionekana kutoliunga mkono wazo hilo la miongo kadhaa la Serikali kwa madai kwamba suala hilo ni kama kiini macho. Kwa mfano Wizara mpya kadhaa zimeanzishwa kwenye awamu hii ya nne na ofisi zao zinajengwa jijini Dar es salaam. Sasa kama kweli serikali ina nia ya dhati kwanini isingejenga ofisi hizo Dodoma?
Kitaalam kila kinachofanyika lazima kipimwe kwanza kabla hakijaanzishwa. Hapa vipimo vinaangalia misingi ya uwezekano, faida na hasara. Kwa vyovyote vile kama hasara ni kubwa basi hatuna budi kuachana na wazo hilo.
Hapa lazima tuwekane sawa kwamba serikali yetu bado inashindwa kufanya upembuzi yakinifu katika kuyaendea mambo. Kwa sababu hata ukimuuliza mtoto wa shule ya msingi akuambie makao makuu ya serikali yalipo, atakujibu Dodoma lakini katika hali ambayo ni ya wasiwasi kwa vile mazingira halisi yanamsuta.
Kwa upande wa nadharia ni kweli kwamba makao makuu ya serikali ni Dodoma, lakini tukirudi kwenye ukweli makao makuu ya serikali yetu ni Dar es salaam. Huko ndiko Ikulu kuu ilipo, ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara zote za Serikali.
Lakini kuna wadau wengine ambao wanasema kwamba fikra za wakuu wetu zimefungwa kwenye imani fulani, fulani hivi ambazo hazina msingi wowote, wala hazina manufaa yeyote kwa nchi yetu ya Tanzania.
Kwa mfano ikiwa kitu alikianzisha Mwalimu Nyerere, basi inakua vigumu sana kukibadili hata kama hakina maana, suala kama hili la kujenga ukumbi mkubwa wa Bunge pale Dodoma kwa kisingizio kwamba ni makao makuu ni miongoni mwa mambo ambayo yanaonyesha utiifu wa kibubusa ndani ya serikali kwa Mzee Nyerere.
Taifa masikini kama Tanzania lilipaswa kufikiria kiasi cha mafuta yanayotumiwa na Waziri Mkuu na Mawaziri wengine kwa mwaka kwenda Bungeni Dodoma na kurudi Dar es salaam ambayo kimsingi yanatokana na kodi za wananchi.
Tukiwatafuta wataalamu wa uchumi wanaweza kutuambia ni bilioni ngapi zinatumika katika utaratibu huu mbaya wa Serikali yetu kwa mwaka. Fedha ambazo zingetumika kuwaletea wananchi maendeleo kwenye sekta mbalimbali.
Pia lazima ifahamike kwamba magari hayo ya kwenda Dodoma pia yanahitaji vipuri ambavyo vinalazimika kubadilishwa mara kwa mara ili kukidhi safari hizo ambazo ni ndefu. Hizi zote ni gharama za kujitakia ambazo kama serikali yetu ingeukubali ukweli, ukweli kwamba Dodoma sio makao makuu fedha zote hizo zingeokolewa.
wakati mwingine safari ya Dodoma kwa viongozi wakuu wa Serikali, inawalazimu kutumia ndege, ndege ambayo kwa vyovyote vile gharama zake ni kubwa sana. Hapa ndipo wachunguzi wa hali ya mambo wanapotuambia kwamba hatutaendelea milele kwa vile hatujui kuangalia mambo ya msingi tukayafanya na kuyaacha yale ambayo hayana msingi.
Lazima pia tutambue kwamba ni hatari kusafiri safari za mbali kama hizi za Dar-Dodoma mara kwa mara. Wengi wetu bado hatujasahau pigo tulilolipata kuondokewa na Waziri Mkuu ambaye alikua mchapa kazi hodari, Waziri aliyeweka rikodi ya uadilifu ambayo mpaka leo haija vyunjwa Bw. M. Sokoine. Kiongozi huyu ni muadhirika wa mzimu wa Makao Makuu ya Dodoma kwavile alipata ajali akiwa anasafiri kutoka Bungeni Dodoma.
Lakini pia tukiangalia kwenye upande wa usalama wa viongozi wetu, makoa haya makuu ya kufikirika kua mbali na makao makuu ya kweli ya Dar es salaam ni hatari kubwa sana. Mathalani kukitokea kikundi cha waasi kikaweka kambi maeneo ya njia kuu ya kwenda Dodoma Bunge litaendelea?
Kwa nchi kama Uganda, Rwanda, Burundi au Kenya kungekua na utaratibu kama huu wa kwetu na siasa zao za kikabila na kulipa visasi kama tunavyozisikia ingekua hatari kubwa. Safari ya Dar-Dodoma ni safari ndefu ambayo ni hatari sana kwa usalama wa viongozi endapo kutakua na mabadiliko ya hali ya mambo.
Suala ambalo linatisha zaidi ni kwamba huenda serikali yetu bado inafikiria namna ya kupata fedha za kujenga majengo kwa ajili ya ofisi na Wizara zote za Serikali kule Dodoma. Sasa siku tukisikia nchi yetu imekopa matrilioni kadhaa kwa ajili hiyo wakati hatuna huduma nyingi za muhimu tusije kushangaa kwa sababu fikra hizi tunazilea wenyewe.
Mimi naiomba serikali yetu iache kungangania fikra ambazo hazina msingi eti kwa sababu zilianzishwa na waanzilishi wa Taifa letu. Lazima tuweze kufanya upembuzi yakinifu na kama tukiona suala halina msingi wowote kama hili la makao makuu Dodoma tuachane nalo.
0 comments on Makao Makuu Dodoma Ni Kiini Macho
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster








