Mjadala wa hotuba ya bajeti unaondelea kwenye Bunge la jamhuri ya Tanzania umetawaliwa na vilio kutoka kwa wabunge kila mmoja akilia na Serikali kwamba Jimbo lake limesahaulika. Wanaikumbusha Serikali kwamba hii ni bajeti ya lala salama, bajeti ambayo ingepaswa kuwa inamaliziamalizia ahadi lukuki zilizotolewa mwaka 2005 wakati ule wa kampeni za kuwania urais, kampeni ambazo zilitawaliwa na ahadi lukuki ambazo pengine hazijawahi kuahidiwa kabla. Wabunge wanakubaliana kwa kauli moja kwamba mkataba wa CCM na wananchi ni Mkataba wa miaka mitano, wala sio mkataba wa miaka kumi kwa kuwa kupata nafasi ya kuongoza tena kwa kipindi kijacho ni jambo lisilokuwa na uhakika kwa kuwa linategemeana sana na maamuzi ya wananchi kipindi hicho kikifika. Wanakumbusha kwamba Rais Kikwete aliahidi kwamba atahakikisha kwamba uchumi wa nchi unakuwa, na kweli unakuwa kitakwimu kwa kuwa mwaka wa fedha uliomalizika 2007/2008 tunaambiwa kwamba umekuwa kwa 7.1%, lakini wakati huohuo maisha yanazidi kuwa jiwe. Ikumbukwe kwamba alichoahidi Rais kikwete ilikuwa ni kukuza uchumi kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja, kwamba kila mtanzania aone fedha mfukoni kwake kwa kuwa miaka yote tumesikia kupanda kwa uchumi kwenye takwimu tu. Hili ni jambo zito ambalo kama halitazingatiwa huenda serikali ya Kikwete ikaingia lawamani mwisho wa siku. Huko Karagwe Mbunge analalamika kwamba jimbo lake limesahaulika, anasema hakuna ulinzi, uwanja wa ndege uliopo ni kama makumbusho kwa kuwa hata Rais alipokwenda huko ndege yake ilishindwa kutua kutokana na ubovu wa uwanja huo, anasema hata mawaziri hawapendi kutembelea huko kwa kuwa hali ya usalama ni mbovu sana na kufanya ziara huko Waziri anahitaji kuwa na ulinzi mzito wa askari zaidi ya wane wenye silaha njito. Anasema suala la mabasi kutekwa na abiria kuibiwa kila kitu ni jambo la kawaida, hata pale ambapo polisi wanaingilia kati bado wanazidiwa nguvu kwa kuwa silaha zao ni nyepesi ukilinganisha na zile za majambazi. Anasema polisi wa jimbo lake wanaishi katika mazingira magumu sana kikazi kiasi cha kuwafanya washimdwe kufanya kazi zao kikamilifu jambo ambalo linaonyesha kwamba Serikali inashindwa kutimiza ahadi yake ya maisha bora kwa kila mtanzania. Mbunge huyo anasema kwamba Karagwe imekuwa kitovu cha majanga ambayo kwa kiasi kikubwa yanairudisha nyuma kimaendeleo na wakati huohuo Serikali inalitupa mkono jimbo hilo. Anasema miaka ya 1970’s vita ya Iddi Amin kagera ndio ilivamiwa na miundombinu yote ikaharibiwa ambayo mpaka leo bado haijarejeshwa katika hali yake ya kawaida, kwenye miaka ya 1990’s Mv bukoba nayo ikazama na ndugu zao kibao wakapoteza maisha, mpaka leo Serikali imeshindwa kuitoa meli hiyo, pia imeshindwa kuweka mikakati ya kununua meli nyingine, anahoji hivi Serikali inasubiri na MV Victoria izame watoe tena pole na kuweka siku ya maathimisho na kujenga mnara mwingine wa kumbukumbu? Anasema balaa la wakimbizi limewaangukia pia, wananchi wanagombania raslimali na wageni ambao pia wanajihusisha na vitendo vya uhalifu, hapa napo anailaumu Serikali kwamba isipolishughulikia vyema hili la wakimbizi hakutakuwa na maisha bora kwa wananchi wa Karagwe. Anakumbusha kwamba Rais kikwete alipotembelea huko kwa ajili ya kampeni za urais mwaka 2005 aliwauliza wananchi wa Karagwe “tukishinda tuwape nini?” wakamwambia barabara, yeye akajibu akawaahidi kwamba wamepata, lakini mpaka leo bajeti ya lala salama bado hakuna dalili za kutekeleza agizo la Rais, yeye anaamini kabisa kwamba ahadi ya Rais ni agizo na amri kwa Mawaziri husika, pia anasema suala la ahadi ya umeme vijijini limebaki ahadi mpaka leo jambo ambalo linatia wasiwasi kwa hali ya baadae ya CCM haswa itakaporudi kwa wananchi kuomba kura. Mbunge mwingine aliyeilalamikia sana Serikali ni yule wa Tarime kwa tiketi ya CHADEMA, anadai kwamba wananchi wake wametengwa, wamefanywa kama Wakenya kwa kuwa Serikali imeweka kizuizi kilometa mia ndani ya Tanzania ambako chakula kwenda upande wa pili wa kizuizi hicho hakiruhusiwi, anahisi kwamba Serikali ya Tanzania inaendesha mambo kwa misingi ya kiubaguzi na haswa ikizingatiwa kwamba wananchi wa jimbo lake ni wapinzani. Hata hivyo kwenye mchango wake alikumbana na vikwazo kadhaa vya muongozo kwa kile kilichodaiwa kwamba anakwenda nje ya hotuba ya Waziri wa Fedha, yeye alijitetea kwamba lazima aseme kwa kuwa wananchi wake ni walipa kodi lakini pia hawawezi kuchangia bajeti wakati wana njaa. Anasema Serikali imewaacha Wakuria wauwame mpaka wamefikia 30 na hakuna anayehangaika kwa madai kwamba kupigana ni jadi ya Wakuria. Hivi kweli Mheshimiwa Spika kuna watu wenye jadi ya kupigana? Alihoji mbunge huyo. Anasema kwamba Serikali imechukua asilimia kubwa ya arthi ya tarime kama hifadhi na kuwanjima kabisa wananchi wa Tarime hata vibali vya kuwinda kwenye hifadhi hizo za taifa, lakini Serikali hiyohiyo inadiriki kugawa arthi kwa wageni kama njugu. Anasema mambo haya na mengine mengi yanamfanya ashindwe kuchangia bajeti ya mwaka 2008/2009 kwa kuwa anahisi kabisa kwamba watu wake hawatendewi haki. Kimsingi maneno ya Mhe. Blandes ambaye ni Mbunge wa Karagwe na Mhe. Wangwe ambaye ni Mbunge wa Tarime yote yanaharufu ya ubaguzi, kwamba sasa wabunge wameanza kupata fikra kwamba Serikali ya Tanzania inawatenga wananchi wake mafungumafungu kwa sababu inazozijua yenyewe. Hili ni jambo hatari sana na lazima Serikali ijizatiti kikamilifu ili iweze kujibu hoja kwa umakini na umahiri ili kuizuia sumu hii isikue. Tanzania ambayo katiba yake inaeleza wazi kwamba ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya kiujamaa ni nchi ambayo inapaswa kuwa na ushirikiano wa dhati kabisa, kuwa na usawa katika nyanja zote, hivyo basi tunaporuhusu mawazo ya kwamba sisi tunatengwa wao wanapendelewa tutafikia pahala nchi hii itashindikana kutawalika kabisa. Serikali ya Rais Kikwete inapozungumzia maisha bora kwa kila Mtanzania, kwanza tunapata picha kwamba watanzania wote tupo sawa kwenye macho ya Serikali bila kujali makabila,rangi wala dini zetu. Hivyo hivyo tunategemea kwamba kila Mtanzania aone kwa vitendo namna ambavyo yeye ni sawa kwenye macho ya Serikali, yaani asitendewe jambo ambalo litamfanya ajihisi mnyonge kwa kuwa kwa kufanya hivyo tunapingana kabisa na katiba ya nchi. Suala la ubaguzi kama huko Zanzibar, limekuwa jambo la kawaida ambalo limezoeleka kwenye masikio ya Wazanzibar na Watanganyika na pengine hata huko nje ya mipaka yetu. Lakini hatusifu kwamba ni vyema Zanzibar ikabaki hivyo na hii ndio maana kumekuwapo juhudi za makusudi kabisa za kumaliza tofauti zilizopo miongoni mwa Wazanzibar, sasa halahala tusije tukageuzia macho upande mmoja kumbe upande wa pili nako kunateketea. Hii inatokana na ukweli kwamba hakuna maana kama tutahangaika na migogoro ya Zanzibar tu na tukasahau kwamba huko Tarime, Karagwe na Kigoma kuna wananchi ambao wanajihisi kabisa kwamba nao wametengwa kama wanavyohisi Wapemba huko Zanzibar, kwa kufanya hivyo mambo yatakuja kutuvimbia tushindwe kuyamaliza. Ni ukweli usiopingika kwamba huko Dafur na Iraq na kwengineko kwenye machafuko, kifo cha mtu mmoja au wawili ni jambo ambalo linatangazwa na vyombovyote vikubwa duniani na kulaaniwa vikali na taasisi na mataifa mbalimbali, lakini ikiwa ni kweli kwamba hapo Tarime ndani ya mipaka yetu wanakufa watu 30 kwa mapigano ya kikabila na Serikali haifanyi chochote ni jambo la kusikitisha sana. Pia ikiwa ni kweli kwamba hapo Tarime yapo maeneo ambako chakula hakifiki kwa kuwa wahusika wanayatazama kama ni ya Kenya kwa sababu tu ya chuki za kisiasa ni jambo la kusikitisha sana na lazima serikali ichukue hatua haraka. Kwa mtindo huu tunajenga Pemba nyingine. Suala la wazawa kuzaraulika kuliko wageni ni suala la kila siku ambalo tumekuwa tukililalamikia siku hadi siku, hata huko Tarime linasemekana lipo kwa madai ya Mbunge wa jimbo hilo ambako wazawa wananyimwa hata vibali vya kuwinda wakati wageni wamepewa maeneo makubwa sana, huko wamejenga mahoteli ambayo hata Wabunge wanazuiwa kuingia, pia kunatetesi kwamba hata viwanja vidogo vya ndege vimejengwa humo ndani kiasi kwamba kunawasiwasi kwamba wageni hao ambao ni wawekezaji wanasafirisha wanyama nje ya nchi kinyemela. Haya ni mambo ya kuyaangalia kwa jicho makini kabisa ili tuhakikishe kwamba nchi yetu inaendelea kuwa na amani na maisha bora kwa kila mtanzanzia yanapatikana haswa ikizingatiwa kwamba muda wa Serikali yenye ilani hiyo ya maisha bora inakaribia kumaliza ngwe yake ya miaka mitano.
0 comments on Karagwe,Tarime ni Pemba ya Tanganyika?
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster








