Jinamizi Litakalo Tuangamiza Tusipokua Makini

June 27, 2007 / by saiboko

Makala hii ilichapishwa kwenye gazeti la fahamu la tarehe 18/06/2007


Dr. Nyindo

“Jamani watumaliza, wadogo hata wakubwa, vifo moja kwa moja, atakaye baki nani? Maofisa wanakwenda, viongozi kadhalika na sisi pia tunafuata” haya ni maneno yaliyopo ndani ya wimbo mmoja unaotoa ujumbe juu ya ukimwi. Sikumbuki ni wimbo wa nani, lakini nakumbuka kwamba niliwahi kuusikia kwenye moja ya redio zetu hapa nchini.

“UKIMWI; kama hujaadhirika, umekuadhiri” haya yalikua menono ya Dr. Mramba, Nyindo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya baiolojia alipokua akiwasilisha mada kwenye chuo cha SUA kule Morogoro. Haya ni maneno mazito sana ambayo yalinifanya niwaze sana.

Dr. Nyindo anasema “mimi ni mzima, nimepima sina virusi. Lakini Ukimwi umeniadhiri sana. Mwaka 1994 kaka yangu alikufa na akaniachia familia, sasa napata taabu kuilea kwa sababu ya UKIMWI”. Kwa maneno haya ndio akatudhibitishia kwamba aidha uwe nao au la, lakini lazima ujue kwamba umekuadhiri.

Utafiti alioufanywa na Dr. Nyindo kule Moshi ambao matokeo yake pia aliyawasilisha pale SUA unaonyesha kwamba wanafunzi wa shule ambazo ziko pembezoni mwa barabara kuu kama ile ya Moshi-Arusha wameadhirika zaidi kuliko wale ambao wako maeneo ya ndani.

Anasema utafiti ulionyesha kwamba, wanafunzi wasichana wameadhirika zaidi kuliko wavulana “wakati wasichana walikua na asilimia 1.3 ya maambukizi, wavulana walikua na asilimia 0.7, Wilaya ya Hai ikiwa na maambukizi kidogo zaidi na Wilaya ya Moshi mjini ikiwa inaongoza. Walioadhirika kwa wingi walikua watoto kuanzia miaka 14-18” alisema Dr. Nyindo.

Alipozungumzia saula la unyanyapaa, alisema kwamba tatizo la Watanzania ni kwamba anapotokea mtu ameadhirika watu wanaanza kuangalia kwanza aliupata vipi? Na wanamtenga kwa vile wanamuona ni mtu aliyefanya dhambi kwa vile mawazo ya watu huwapelekea kuamini kwamba kila mwenye Ukimwi ameupata kwa njia ya ngono.

“sio wakati muafaka kuangalia mtu aliupata wapi, ila tunatakiwa tuangalie namna ya kumsaidia ili aweze kuishi muda mrefu zaidi” alisema Dr. Nyindo

Pia aliongeza kusema kwamba ukimwi una aina mbalimbali, na ndio maana waadhirika wanaambiwa wasifanye ngono ovyo kuwakomoa watu au kwa lengo la kuwaambukiza wengine kwa sababu kuna hatari ya kupata virusi vya aina tofauti ndani ya mwili wa mtu mmoja jambo ambalo ni hatari sana.

Anasema kwamba huenda mtu ambaye atapata virusi wa aina tofauti wa ukimwi hataweza kuishi kwa muda mrefu kwa sababu atashambuliwa kwa kasi ya ajabu na uwezekano wa kusaidiwa na ARV’s (dawa za kurefusha maisha) hautakuwepo tena.

“Ukimwi uko wa aina nyingi, kuna (B), (C), (C,E), na (ACD). Sasa inapotokea virusi vikakutana kwenye mwili wa mtu mmoja inakua hatari. Ndio maana inakua vigumu kubuni dawa ya Ukimwi kwa vile virusi vyake viko vya aina tofauti” alisema Dr. Nyindo

Alipo ongelea suala la matibabu, alisema kwamba dawa za kupunguza makali zipo, lakini akasisitiza pia kwamba dawa hizo ni mbaya sana na zinaumiza na kutesa sana. Anasema wagonjwa wote wanaozitumia wanalalamika zinavyo waumiza, kwa hiyo akasema cha muhimu ni kujitahidi kuhakikisha kwamba haupati ugonjwa huo.

“dawa ni kali sana, watu wengine wanakataa na wanatamani kufa kuliko kuendelea kuzitumia dawa hizo. Pia zina madhara makubwa mwilini kama vile kukausha mafuta” alisema Dr. Nyindo

Pamoja na ugonjwa huo kuonekana kuwa hatari zaidi, Dr. Nyindo anasema bado ugonjwa huo unashikilia nafasi ya nne kwenye orodha ya magonjwa yanayo ua zaidi duniani. Kwa mfano alisema malaria inaua zaidi kuliko Ukimwi na kwamba kila dakika tatu mtoto mmoja wa Kiafrika anafariki dunia kwa malaria.

Hii inamaanisha kwamba pengine waafrika hufa kwa wingi zaidi kwa Ukimwi kwa sababu za kuchanganya magonjwa. Kwa mfano wengi wanakua na Malaria na wakati huo huo wana virusi vya ukimwi jambo ambalo linawapelekea kupoteza maisha kwa haraka zaidi.

Lakini pamoja na kuifahamu hali halisi kama alivyo ieleza Dr. Nyindo na wataalamu wengine tangu Ukimwi ulipo ingia nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1981, bado maambukizi yanaongezeka siku hadi siku. Matangazo ya kuhimiza watu kuepuka gonjwa hili yamekua mengi sana kiasi kwamba kila kona ya mji yapo. Kondom zimezagaa mpaka zinagawiwa bure lakini bado Ukimwi unazidi kushamiri.

Haya ni mambo ambayo yanawachanganya wataalamu, kwa sababu tulitegemea kwamba wingi wa matangazo na wingi wa semina ambazo zinafanyika kila siku na pia wingi wa misaada ya kupambana na ukimwi iwe kama chachu ya kupunguza maambukizi. Lakini bado ukimwi unaongezeka kwa kasi ya ajabu.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kuchunguza hali halisi ya Ukimwi mwaka 2003/2004 unaonyesha kwamba watu wengi wanajua ukimwi ni nini na unazuilika vipi. Utafiti huo unaonyesha kwamba “ asilimia 99 ya watanzania wa Tanganyika wenye umri kati ya miaka 15-49 wamewahi kusikia kuhusu Ukimwi” hii ni sababu tosha yakujitapa na kujidai kwamba Taifa letu limefanikiwa sana kuelimisha watu. Lakini matokeo yake hayafanani na kazi iliyofanyika.

Lakini pia kuna nchi kama zile za Uarabuni ambazo zinaukiritimba, ukiritimba kwa sababu zimekataa kujiunga na kampeni za kutangaza na kuhimiza matumizi ya kondomu. Badala yake zimekua zikihimiza zaidi vijana waoe na kuolewa kwenye umri mdogo mara baada ya kubaleghe. Kitendo hicho kimesaidia mataifa hayo kupunguza sana maambukizi ya ukimwi.

Nchi kama Algeria, Saudi Arabia, Afghanistan, Kuwait, Qatar na Oman ambazo zinasememekana kua na ukiritimba (conservativeness) zimefanikiwa sana kuudhibiti ukimwi kwa kua na asilimia 0.1 tu ya maambukizi. Tofauti na nchi nyingine za Afrika ambazo zinasemekana kua vinara wa kampeni dhidi ya ukimwi kama vile Tanzania, Kenya, Botswana, Ethiopia, Lesotho, na nyinginezo ambako matumizi ya kondom au ngono salama yanasisitizwa.

Taarifa zinaonyesha kwamba Zimbabwe imefanikiwa kufanya kampeni dhidi ya ukimwi kwa muda mrefu sasa na kondomu zipatazo milioni 259 zimesambazwa. Pia inasemekana kwamba kondomu hizo zinanunuliwa na wananchi wanamuamko mkubwa na wanazitumia sana.

Kulingana na taarifa iliyotolewa kwenye siku ya ukimwi duniani mwaka 2006, kinchi kidogo cha Lesotho kina wagonjwa wengi kiasi ambacho kwenye kila watu wazima watatu, mmoja ameadhirika. Pia taarifa hiyo ilisema kwamba Swaziland ina waadhirika wanne katika kila watu kumi, wakati Afrika Kusini ina asilimia 20 ya waadhirika kwenye wananchi wenye umri wa kuanzia miaka 15-49.

Taarifa iliyotolewa na Marekani mwaka 2003 inaonyesha kwamba ongezeko la watu wazima wanaopata ukimwi Tanzania ni asilimia 8.8. ambayo inaiweka Tanzania kwenye nafasi ya 12 kwenye dunia kwa kua na maambukizi makubwa. Wakati huohuo taarifa hiyo ilionyesha kwamba Saudi Arabia na Afghanistan ina asilimia 0.01 na wengi miongoni mwa walioadhirika ni wageni na wananchi ambao wamewahi kuishi nje ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa gazeti moja la kila wiki la kiiengereza la hapa nchini. Nimarufuku kuzungumza kuhusu Kondomu na matumizi yake huko Algeria na imekua zoezi gumu sana kuwahimiza watu juu ya matumizi yake. Pia taarifa hiyo ilisema kwamba nchi hiyo ina Kondom nyingi sana lakini hakuna wanunuzi.

Wakati taarifa za uchunguzi zinaonyesha kwamba idadi ya kondomu zinazouzwa nchini Tanzania kwenye kipindi cha miaka mitano imeongezeka kutoka Milioni 40 mwaka 2001 mpaka milioni 180 mwaka 2006. Taarifa ya TACAIDS kwenye toghuti yao inaonyesha kwamba ukimwi unaongezeka kwa kasi nchini mpaka kufikia asilimia 10 kwenye maeneo ambayo watu wanafanya sana ngono. Hizi ni taarifa ambazo hazikutegemewa ukilinganisha na juhudi zinazo fanyika.

Hii inaonyesha kwamba tusipokua macho ukimwi utatumaliza. Tatizo lililopo kwenye matumizi ya kondomu tukiachilia mbali shutuma kwamba hazina uwezo wa kuzuia maambukizi ni kwamba watumiaji wenyewe wana matatizo. Kwa mfano mlevi wa pombe anaweza kutumia kondom akishalewa? Hata kama ataitumia hawezi kuitumia ipasavyo. Kwa hiyo ulevi nao unachangia kuongeza maambukizi.

Rais Kikwete ameonyesha nia ya kuwasaidia wananchi waliodhirika. Lakini kubwa zaidi ni adhima ya serikali yake kutunga sheria ya kuwadhibiti watu wanaosambaza ukimwi kwa makusudi. Haya aliyasema kwenye hotuba yake ya tarehe 6/6/07 alipoongea na wahariri Ikulu. Ni jukumu letu kumuunga mkono Rais ili tupunguze maambukizi mapya na tusiwatenge waadhirika kwa sababu huenda ndio maana wanausambaza.

0 comments on Jinamizi Litakalo Tuangamiza Tusipokua Makini

Add a comment

To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster

  • Type the words in the box below the image.

Email this blog post to a friend

To email posts to friends, you must be logged in. Login or Join Blogster

Friends

View All