Mpendwa mwaka 2008, ninakupongeza,. nakupongeza kwa kuwa umeniletea zawadi za ushindi, umekuwa tofauti kabisa na wenzako, wao walikosa mvuto na kuninyima kabisa matumaini. Naam lazima nikupongeze, nikupongeze kwa kuwa pamoja na uchanga wako umeweza kufungua ukurasa mpya kwenye siasa za nchi yetu, nchi yangu niipendayo ya Tanzania ambayo kwa muda mrefu sasa imetambulika kama kisiwa cha amani Afrika na duniani kote. Kisiwa cha amani ambacho wakazi wake wanataabika kwa njaa na shida za kila aina jambo ambalo linanifanya niamini kabisa kwamba kwenye njaa hakuna amani.
Lowassa
Wakati tunakuna vichwa kujiuliza kulikoni Tanzania yenye neema inafikia hatua ya hatihati ya kushindikana? Mara mwishoni mwa mwaka 2007 kukazuka msamiati ufisadi, alaa hapa ndio tukaanza kupata picha pengine ufisadi ndio tatizo letu, lakini vita hiyo ya kuwamulika mafisadi wakati ule ikawa ngumu, tuliowategemea kutukomboa kama Wabunge ambao ndio wenye wajibu wa kuisimamia Serikali nao wakawakumbatia mafisadi, wakati ule wengine walisimama na kukemea lakini baadae mara nao wakawa kimya, tusijue eti kumbe walizibwa midomo, mwingine kutoka kambi ya upinzani akasimamishwa kuhudhuria shughuli za bunge kwa muda mrefu kidogo, wengine wakatoa hoja zao Bungeni wakatuletea huku mtaani kwa kuwa walihofia kuadabishwa kama mwenzao.
Baada ya kuwa tumepata taarifa zote na mafisadi wakatajwa hadharani, bado kukawa kunakosekana nguvu ya kuwawajibisha hao waliokuwa wanaitwa mafisadi, sisi wenye silaha za kalamu tukaendelea kuandika, tuliandika tukisisitiza kwamba shutuma zile hazikuwa tupu, tulijua kwamba kuna kitu, hata hivyo tukapata wakati mgumu kidogo kwa kuwa hakukuwa na wakutusikiliza. Wakati ule hata Rais Jakaya Mrisho Kikwete alihojiwa juu ya umasikini wa nchi yetu, akasema anashangaa kwanini Taifa letu ni masikini, Rais alishangaa kwa kuwa Taifa hili linakila sababu ya kuwa tajiri kutokana na raslimali ambazo zipo.
Naama wakati tunatafakari kwamba iweje hata Rais haelewi kwanini nchi ni masikini mara taarifa rasmi ya ukaguzi wa akaunti ya madeni ya nje (EPA) kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikakabithiwa kwa Rais Kiwete, taarifa ile ikamstua Rais na mstuko ule ukampelekea kupitisha maamuzi mazito ya kumfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa BoT Bwana Daudi Balali, wananchi tukafurahia uamuzi ule kwa kuwa ulikuwa unalenga kutupatia majibu ya tatizo la umasikini nchini. Kwangu hiyo ilikuwa zawadi ya kwanza ya Mwaka 2008, mwaka ambao nauona umeanza na matumaini makubwa kwangu na taifa kwa ujumla. Baada ya pale tukatambua kwamba kumbe ule ufisadi uliokuwa unazungumziwa BoT ulikuwa wa kweli.
Lakini wakati tunafuatilia kwa karibu kuona jinsi ambavyo washirika wa Balali watakavyopatikana na kufikishwa kwenye mikono ya sheria, mwaka 2008 ukaleta zawadi nyingine kupitia Tume ya Mheshimiwa Harrison Mwakyembe (Mbunge wa Kyela CCM) ambayo ilichukua dhima ya kuchunguza mkataba wenye utata wa Richmond, mkataba uliokuwa ukililiwa na wanaharakati kwamba umejaa uchafu mwingi ndani yake. Tume ile ilibainisha machafu mengi ambayo singependa kuyataja hapa kwa kuwa siwezi kuyamaliza, lakini pia naamini kabisa Watanzania amboa wamekuwa makini kwenye mchakato wote huu wanayafahamu vizuri mambo hayo yaliyobainishwa na Tume ya Mwakyembe.
Siku moja baada ya kuwasilishwa Bungeni matokeo ya Tume hiyo, Mwaka 2008 ukaandika historia nyingine ambayo ni zawadi kwa Watanzania, naam zawadi ya kujiuzulu kwa watuhumiwa wakuu watatu (aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Naziri Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki Ibrahim Msabaha), hii ni zawadi kubwa ndani ya 2008 kwa kuwa imegusa suala la msingi kabisa ambalo kwetu limekuwa gumu sana, suala la kujiuzulu. Mtu kama Karamagi tangu aanze kutajwa kwenye ufisadi kwakweli hatukutegemea kwamba angesubiri mpaka hivi majuzi, kimsingi amejiuzulu kwa kuchelewa sana.
Edward Lowassa amezungumzwa vibaya sana kwa kuwa watu wanaamini kabisa kwamba alihusika kwa namna moja au nyingine, lakini pia wananchi na viongozi kwa ujumla wamempongeza kwa kujiuzulu, tunaweza kusema kwamba Lowassa ameonyesha uzalendo wa hali ya juu, lakini kumbe angefanyaje? Maji yalishafika shingoni, kama ni taulo lilishavutwa, kumbe angefanya nini kama si kuchutama? ingekuwa nchi hii kila anayetajwa kwenye ufisadi anajiuzulu mara moja ingekuwa ni jambo la busara sana, hata hivyo pamoja na kwamba Lowassa ameonyesha njia, lakini namna alivyojiuzulu inatia mashaka na kwa maneno mengine ni namna ambayo inakereketa kidogo, amejiuzulu huku akiwa analia moyoni mwake, analia anasema ameonewa sana, anasema anaona tatizo ni Uwaziri Mkuu, anamaanisha Mwakyembe na tume yake wanamuonea donge kwa nafasi yake, lakini ili kukata mzizi wa fitna ameamua kujiuzulu. Wananchi nao wanasema potelea mbali ufisadi umetutesa sana.
Ukweli ni kwamba bado viongozi wetu hawajafikia hatua ya uzalendo wa dhati, hawajafikia hatua ya kuona kwamba madaraka ni hatari, kwamba madaraka ni kitu cha kukiogopa kwa kuwa kinakubebesha lawama, badala yake wenzetu hawa wakipata nafasi kama za Uwaziri wanachekelea, wanachekelea kwa kuwa wanafikiri kwamba uwaziri ni nafasi pekee ya kujitajirisha, kwenye uwaziri ndiko kwenye mikataba ya mabilioni, ndiko kwenye anasa za magari ya kifahari, nyumba za kifahari na marupurupu ya kila aina. Mambo haya ndio wenzetu wanayaangalia mwanzo, hawajishughulishi na kuwaza namna ya kuwatumikia wananchi, ndio tumefikia hapo mtu anashutumiwa analalamika anafikiri eti ameonewa donge, anafikiri wenzake wanaitaka nafasi yake ili nao wafaidi.
Mawaziri wengine waliojiuzulu baada ya Lowassa (Karamagi na Msabaha) nao wamejiuzulu kwa kulalamika sana, nao wanahisi wameonewa kwa namna moja ama nyingine, ilifikia pahala Karamagi anasema eti anajitoa kafara, wakati Msabaha naye alisema kuiambia tume kwamba yeye atakuwa kondoo wa kafara, hawa ni watu wawili ambao mmoja amesaini mkataba, baadae akahamishwa Wizara, mwingine amehamishiwa Wizara na akendelea kuulinda mkataba na kufikia hatua ya kuuhamishia kwa kampuni jengine. Wote wanasema wametolewa kafara na kwa hiyo wameamua kujiuzulu. Maneno haya ya “tumetolewa kafara” “nimejitoa kafara” “kondoo wa kafara” huenda yanamaana nzito ndani yake. Laiti wahusika wangesema ukweli wa kile wanachokikusudia Watanzania tungejua mengi zaidi kuhusu mkataba wa Richmond.
Suala la msingi hapa ambalo tumejifunza ni kwamba watu hawa wamejiuzulu shingoupande, bado wanahisi kabisa kwamba hawakutendewa haki, kutokana na ukweli huu suala hili linapashwa kabisa kupelekwa kwenye hatua nyingine kama walivyoshauri baadhi ya Wabunge na Wananchi kwamba ipo haja ya makusudi kabisa ya kuwapeleka mahakamani wahusika hawa ili wakapate haki yao ambayo wanahisi wamenyimwa kwenye uchunguzi wa tume ya Mwakyembe, kama wakikutwa na makosa basi wachukuliwe hatua zaidi. Lakini pia wahojiwe watuambie nani kawatoa kafara? Je wao walishurutishwa na nani? Au walipitiwa na kujikuta wanatamka mambo bila ya kujitambua? Haya yatafahamika huko.
Lazima tutambue kwamba viongozi hawa hawakupenda kujiuzulu, ukweli huu tunaweza kuuona kwenye maneno yao ya mwisho Bungeni wakiwa kama Mawaziri kabla ya kujiuzulu, kimsingi haikutakiwa kuwa vile na kwa namna ile hawa tunaweza kusema kwamba walishagundua kwamba kifo kipo karibu na hivyo wakaamua kujiua mapema kabla siku ya hukumu haijafika. Wangekuwa wazalendo wa kweli wangekwisha jiuzulu siku nyingi zilizopita, pengine tangu mwaka jana kwa kuwa mambo haya ya Richmond yalishasemwa sana na wahusika walikuwa wakitajwa mara kwa mara hata kwenye vyombo vya habari lakini wao wakaendelea kuuma meno, wakajitia upofu na uziwi mpaka imefikia mahali wakavuliwa mataulo yao ndio wakaona aibu kumfukuza aliyewavua na wakaamua kuchutama.
Wakati Lowassa anasema alitafakari kwa kina akaamua kujiuzulu, taarifa zinasema kwamba alishauriwa kufanya hivyo. Huu ndio ukweli ambao tunaweza kuuona waziwazi, kwa kuwa mtu aliyeamua kujiuzulu hawezi kulalamika kiasi kile, malalamiko yale ni ishara tu kwamba walinyang’anywa tonge mdomoni.
Rais kikwete amebainisha kabisa kwamba uwajibikaji wa Serikali yake ulikuwa mbovu sana, na akaonya kwamba “kula nchi sio kazi ya Waziri”, anakiri kwamba baraza lake la Mawaziri lilokuwa linaongozwa na Lowassa lilifanya kazi chini ya matarajio yake. Hizi ni shutuma nzito kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi ambaye pia hakuridhishwa na utendaji wa akina Karamagi.
Bila shaka wakati umefika sasa kwa shughuli mbalimbali za Baraza la Mawaziri kufanyika kwa uwazi zaidi. Maneno ambayo yapo kwenye kiapo cha Mawaziri yasemayo “kwa vyovyote vile sitatoa siri za Baraza la Mawaziri” yanatia wasiwasi kwa kuwa siri hizo hazifahamiki ni zipi hashwa. Je hata mikataba ni siri za Baraza la Mawaziri? Kama hivyo ndivyo basi kuna kila sababu ya kukibadilisha kiapo hicho kwa sababu ni usiri huu ambao unawafanya wenzetu hawa wawe na “ujasiri wa kifisadi”, wanakuwa na ujasiri huo kwa kuwa hakuna wa kuhoji haswa ikizingatiwa kwamba mikataba inafichwa na hivyo kuwafanya wananchi wasijue kinachoendelea.
Suala la msingi hapa ni kwamba Tume ya Mwakyembe imetufungulia ukurasa mpya kwenye siasa za nchi yetu, moto uliowaka Bungeni ni ishara kwamba Bunge sasa limeanza kutekeleza wajibu wake kikamilifu, moto huu usiishie hapa kwenye Richmond bali uendelee mpaka BoT, Buzwagi, IPTL na mikataba mingineyo ili tuisafishe nchi yetu kutoka kwenye mikono ya mafisadi wachache wanao kula nchi.
0 comments on Ahsante 2008 kwa zawadi
Add a comment
To add comments without entering your email and image verification, you must be logged in. Login or Join Blogster









